2 Kor 8:16-24
2 Kor 8:16-24 SUV
Lakini ahimidiwe Mungu atiaye bidii ile ile kwa ajili yenu katika moyo wa Tito. Maana aliyapokea kweli yale maonyo; tena, huku akizidi kuwa na bidii, alisafiri kwenda kwenu kwa hiari yake mwenyewe. Na pamoja naye tukamtuma ndugu yule ambaye sifa zake katika Injili zimeenea makanisani mwote. Wala si hivyo tu, bali alichaguliwa na makanisa asafiri pamoja nasi katika jambo la neema hii, tunayoitumikia, ili Bwana atukuzwe, ukadhihirike utayari wetu. Tukijiepusha na neno hili, mtu asije akatulaumu kwa habari ya karama hii tunayoitumikia; tukitangulia kufikiri yaliyo mema, si mbele za Bwana tu, ila na mbele ya wanadamu. Nasi pamoja nao tumemtuma ndugu yetu tuliyemwona mara nyingi katika mambo mengi kuwa ana bidii, na sasa ana bidii zaidi sana kwa sababu ya tumaini kuu alilo nalo kwenu. Basi mtu akitaka habari za Tito, yeye ni mshirika wangu, na mtenda kazi pamoja nami kwa ajili yenu; tena akitaka habari za ndugu zetu, wao ni mitume wa makanisa, na utukufu wa Kristo. Basi waonyesheni mbele ya makanisa hakika ya upendo wenu, na ya kujisifu kwetu kwa ajili yenu.