Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Nya 20:2-21

2 Nya 20:2-21 SUV

Wakaja watu waliomwambia Yehoshafati, wakisema, Wanakuja jamii kubwa juu yako watokao Shamu toka ng’ambo ya bahari; na tazama, wako katika Hasason-tamari (ndio En-gedi). Yehoshafati akaogopa, akauelekeza uso wake amtafute BWANA; akatangaza mbiu ya watu kufunga katika Yuda yote. Yuda wakakusanyika pamoja ili wamtafute BWANA; hata kutoka miji yote ya Yuda wakaja kumtafuta BWANA. Yehoshafati akasimama kati ya kusanyiko la Yuda na Yerusalemu, nyumbani mwa BWANA, mbele ya ua mpya; akasema, Ee BWANA, Mungu wa baba zetu, si wewe uliye Mungu mbinguni? Tena si wewe utawalaye falme zote za mataifa? Na mkononi mwako mna uweza na nguvu, asiweze mtu ye yote kusimama kinyume chako. Si wewe, Ee Mungu wetu, uliyewafukuza wenyeji wa nchi hii mbele ya watu wako Israeli, ukawapa wazao wa Ibrahimu rafiki yako hata milele? Nao walikaa humo, wamekujengea patakatifu pa jina lako humo, wakisema, Yakitujia mabaya, upanga, hukumu, au tauni, au njaa, tutasimama mbele ya nyumba hii, na mbele zako, (maana jina lako limo katika nyumba hii), na kukulilia katika shida yetu, nawe utasikia na kuokoa. Na sasa, tazama, wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, ambao hukuwaacha Israeli waingie katika nchi yao, walipotoka nchi ya Misri; lakini wakawageukia mbali, wasiwaharibu; tazama, jinsi wanavyotulipa, wakija kututupa toka milki yako, uliyoturithisha. Ee Mungu wetu, je! Hutawahukumu? Maana sisi hatuna uwezo juu ya jamii kubwa hii, wanaotujia juu yetu; wala hatujui tufanyeje; lakini macho yetu yatazama kwako. Wakasimama Yuda wote mbele za BWANA, pamoja na wadogo wao, na wake zao, na watoto wao. Ndipo Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi, wa wana wa Asafu, akajiliwa na roho ya BWANA, katikati ya kusanyiko; akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; BWANA awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya Mungu. Kesho shukeni juu yao; tazameni, wanakwea kwa kupandia Sisi; nanyi mtawapata penye mwisho wa bonde, mbele ya jangwa la Yerueli. Hamtahitaji kupigana vita, jipangeni, simameni, mkauone wokovu wa BWANA ulio pamoja nanyi, enyi Yuda na Yerusalemu; msiogope, wala msifadhaike; kesho tokeni juu yao; kwa kuwa BWANA yu pamoja nanyi. Yehoshafati akainama kichwa, kifulifuli; wakaanguka mbele za BWANA Yuda wote na wakaao Yerusalemu, wakimsujudia BWANA. Na Walawi, wa wana wa Wakohathi na wa wana wa Wakorahi, wakasimama ili wamsifu BWANA, Mungu wa Israeli, kwa sauti kuu sana. Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa. Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia BWANA, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema, Mshukuruni BWANA; kwa maana fadhili zake ni za milele.

Soma 2 Nya 20

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 2 Nya 20:2-21

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha