Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Nya 20:14-30

2 Nya 20:14-30 SUV

Ndipo Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi, wa wana wa Asafu, akajiliwa na roho ya BWANA, katikati ya kusanyiko; akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; BWANA awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya Mungu. Kesho shukeni juu yao; tazameni, wanakwea kwa kupandia Sisi; nanyi mtawapata penye mwisho wa bonde, mbele ya jangwa la Yerueli. Hamtahitaji kupigana vita, jipangeni, simameni, mkauone wokovu wa BWANA ulio pamoja nanyi, enyi Yuda na Yerusalemu; msiogope, wala msifadhaike; kesho tokeni juu yao; kwa kuwa BWANA yu pamoja nanyi. Yehoshafati akainama kichwa, kifulifuli; wakaanguka mbele za BWANA Yuda wote na wakaao Yerusalemu, wakimsujudia BWANA. Na Walawi, wa wana wa Wakohathi na wa wana wa Wakorahi, wakasimama ili wamsifu BWANA, Mungu wa Israeli, kwa sauti kuu sana. Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa. Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia BWANA, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema, Mshukuruni BWANA; kwa maana fadhili zake ni za milele. Nao walipoanza kuimba na kusifu, BWANA akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa. Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwaondokea wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakajitia kuharibu kila mtu mwenziwe. Hata Yuda walipofika mnara wa kulindia wa jangwani, wakalitazama hilo jeshi; nao, angalia, walikuwa maiti walioanguka nchi, wala hapana aliyeokoka. Nao Yehoshafati na watu wake walipokuja kuchukua nyara zao, wakaona kati yao wingi wa mali, na mavazi, na johari za thamani, walivyojivulia, zaidi kuliko wawezavyo kuchukua; wakawa siku tatu katika kuteka nyara, maana zilikuwa nyingi sana. Hata siku ya nne wakakusanyika katika bonde la Baraka; maana ndipo walipombarikia BWANA; kwa hiyo jina lake mahali pale pakaitwa Bonde la Baraka hata leo. Kisha wakarudi, kila mtu wa Yuda na Yerusalemu, na Yehoshafati mbele yao, ili kuurudia Yerusalemu kwa furaha; kwa kuwa BWANA amewafurahisha juu ya adui zao. Wakafika Yerusalemu wenye vinanda vinubi na mapanda kwenda nyumbani kwa BWANA. Ikawa hofu ya Mungu juu ya falme zote za nchi, waliposikia ya kuwa BWANA amepigana juu ya adui za Israeli. Basi ukatulia ufalme wake Yehoshafati; kwa sababu Mungu wake alimstarehesha pande zote.

Soma 2 Nya 20

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 2 Nya 20:14-30