1 Tim 6:1-21
1 Tim 6:1-21 SUV
Wo wote walio chini ya kongwa, hali ya utumwa, na wawahesabie bwana zao kuwa wamestahili heshima yote, jina la Mungu lisitukanwe wala mafundisho yetu. Na wale walio na bwana waaminio wasiwadharau kwa kuwa ni ndugu; bali afadhali wawatumikie, kwa sababu hao waishirikio faida ya kazi yao wamekuwa wenye imani na kupendwa. Mambo hayo uyafundishe na kuonya. Mtu awaye yote akifundisha elimu nyingine, wala hayakubali maneno yenye uzima ya Bwana wetu Yesu Kristo, wala mafundisho yapatanayo na utauwa, amejivuna; wala hafahamu neno lo lote; bali ana wazimu wa kuwazia habari za maswali, na mashindano ya maneno, ambayo katika hayo hutoka husuda, na ugomvi, na matukano, na shuku mbaya; na majadiliano ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida. Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi. Bali wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole. Piga vita vile vizuri vya imani; shika uzima ule wa milele ulioitiwa, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi. Nakuagiza mbele za Mungu anayevihifadhi hai vitu vyote, na mbele za Kristo Yesu, aliyeyaungama maungamo mazuri yale mbele ya Pontio Pilato, kwamba uilinde amri hii pasipo mawaa, pasipo lawama, hata kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo; ambako yeye kwa majira yake atakudhihirisha, yeye aliyehimidiwa, Mwenye uweza peke yake, Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana; ambaye yeye peke yake hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata milele. Amina. Walio matajiri wa ulimwengu wa sasa uwaagize wasijivune, wala wasiutumainie utajiri usio yakini, bali wamtumaini Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha. Watende mema, wawe matajiri kwa kutenda mema, wawe tayari kutoa mali zao, washirikiane na wengine kwa moyo; huku wakijiwekea akiba iwe msingi mzuri kwa wakati ujao, ili wapate uzima ulio kweli kweli. Ee Timotheo, ilinde hiyo amana; ujiepushe na maneno yasiyo ya dini, yasiyo na maana, na mashindano ya elimu iitwayo elimu kwa uongo; ambayo wengine wakiikiri hiyo wameikosa Imani. Neema na iwe pamoja nanyi.