1 Sam 10:1-6
1 Sam 10:1-6 SUV
Ndipo Samweli akatwaa kichupa cha mafuta, akayamimina kichwani pake, akambusu, akasema, Je! BWANA hakukutia mafuta [uwe mkuu juu ya watu wake Israeli? Nawe utamiliki watu wa BWANA, na kuwaokoa na mikono ya adui zao; kisha hii itakuwa ishara kwako ya kuwa BWANA amekutia mafuta] uwe mkuu juu ya urithi wake. Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na wanaume wawili karibu na kaburi la Raheli, katika mpaka wa Benyamini huko Selsa; nao watakuambia, Punda hao uliokwenda kuwatafuta wameonekana; na tazama, baba yako ameacha kufikiri habari za punda, anafikiri habari zenu, akisema, Nifanye nini kwa ajili ya mwanangu? Kisha utakwenda mbele kutoka hapo, na kufika kwa mwaloni wa Tabori, na hapo watu watatu watakutana nawe, wanaokwea kumwendea Mungu huko Betheli, mmoja anachukua wana-mbuzi watatu, na mwingine anachukua mikate mitatu, na mwingine anachukua kiriba cha divai; nao watakusalimu na kukupa mikate miwili; nawe utaipokea mikononi mwao. Baada ya hayo utafika Gibea ya Mungu, hapo palipo na ngome ya Wafilisti; kisha itakuwa, utakapofika mjini, utakutana na kundi la manabii wakishuka kutoka mahali pa juu, wenye kinanda, na tari, na kinubi, na filimbi mbele yao, nao watakuwa wakitabiri; na roho ya BWANA itakujilia kwa nguvu, nawe utatabiri pamoja nao, nawe utageuzwa kuwa mtu mwingine.