Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Pet 2:11-25

1 Pet 2:11-25 SUV

Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho. Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa. Tiini kila kiamriwacho na watu, kwa ajili ya Bwana; ikiwa ni mfalme, kama mwenye cheo kikubwa; ikiwa ni wakubwa, kama wanaotumwa naye ili kuwalipiza kisasi watenda mabaya na kuwasifu watenda mema. Kwa sababu ndiyo mapenzi ya Mungu, kwamba kwa kutenda mema mzibe vinywa vya ujinga vya watu wapumbavu; kama walio huru, ila wasioutumia uhuru huo kwa kusitiri ubaya, bali kama watumwa wa Mungu. Waheshimuni watu wote. Wapendeni ndugu. Mcheni Mungu. Mpeni heshima mfalme. Enyi watumishi, watiini bwana zenu kwa hofu nyingi, sio wao walio wema na wenye upole tu, bali nao walio wakali. Maana huu ndio wema hasa, mtu akivumilia huzuni kwa kumkumbuka Mungu, pale ateswapo isivyo haki. Kwa maana ni sifa gani kustahimili, mtendapo dhambi na kupigwa makofi? Lakini kustahimili, mtendapo mema na kupata mateso, huu ndio wema hasa mbele za Mungu. Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake. Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake. Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki. Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa. Kwa maana mlikuwa mnapotea kama kondoo; lakini sasa mmemrudia Mchungaji na Mwangalizi wa roho zenu.