1 Fal 6:19-38
1 Fal 6:19-38 SUV
Akaweka tayari chumba cha ndani katikati ya nyumba ndani, ili atie humo sanduku la agano la BWANA. Na ndani yake chumba hicho cha ndani mlikuwa na nafasi, mikono ishirini urefu, na mikono ishirini upana, na mikono ishirini kwenda juu kwake; akaifunika na dhahabu safi. Akaifunika madhabahu nayo kwa mwerezi. Hivyo Sulemani akaifunika nyumba ndani kwa dhahabu safi. Akaitenga kwa mikufu ya dhahabu mbele ya chumba cha ndani; akapafunika na dhahabu. Akaifunika nyumba yote kwa dhahabu, hata ilipokwisha nyumba yote; tena madhabahu yote iliyokuwa ya chumba cha ndani akaifunika kwa dhahabu. Akafanya ndani ya chumba cha ndani makerubi mawili ya mzeituni, kwenda juu mikono kumi. Na bawa moja la kerubi lilikuwa mikono mitano urefu wake, na bawa la pili la kerubi mikono mitano; mikono kumi toka mwisho wa bawa moja hata mwisho wa bawa la pili. Na kerubi la pili lilikuwa mikono kumi; makerubi yote mawili walikuwa ya cheo kimoja na namna moja. Kwenda juu kwake kerubi moja kulikuwa mikono kumi, na kerubi la pili vivyo. Akayaweka hayo makerubi katika nyumba ya ndani; na mabawa ya makerubi yakanyoshwa, bawa la moja likafika ukutani huko, na bawa la kerubi la pili likafika ukutani huko; mabawa yao yakagusana katikati ya nyumba. Akayafunika makerubi kwa dhahabu. Akazinakshi kuta zote za nyumba kwa nakshi za makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, pande za ndani na nje. Na sakafu ya nyumba akaifunika na dhahabu ndani na nje. Akayafanyia maingilio ya chumba cha ndani milango ya mzeituni; kizingiti na miimo ilikuwa ya pande tano. Hivyo akafanya milango miwili ya mzeituni; akanakshi juu yake nakshi za makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, akaifunika kwa dhahabu; akatia dhahabu juu ya makerubi, na juu ya mitende. Ndivyo alivyoyafanyia maingilio ya hekalu miimo ya mzeituni, yenye pande nne; na milango miwili ya mberoshi; mbao mbili za mlango mmoja zilikuwa za kukunjana, na mbao mbili za mlango wa pili za kukunjana. Akanakshi juu yake makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi; akazifunika kwa dhahabu iliyonyoshwa juu ya machoro. Akaijengea behewa ya ndani safu tatu za mawe ya kuchongwa, na safu moja ya mihimili ya mierezi. Katika mwaka wa nne nyumba ya BWANA ilitiwa msingi, katika mwezi wa Zivu. Hata katika mwaka wa kumi na mmoja, katika mwezi wa Buli, ndio mwezi wa nane, nyumba ikaisha, mambo yake yote, na sharti zake zote. Basi muda wa miaka saba alikuwa katika kuijenga.