Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Fal 3:1-15

1 Fal 3:1-15 SUV

Huyo Sulemani akafanya ujamaa na Farao, mfalme wa Misri, akamwoa binti yake Farao, akamleta mjini mwa Daudi, hata alipokwisha kuijenga nyumba yake, na nyumba ya BWANA, na ukuta wa kuuzunguka Yerusalemu. Ila watu walikuwa wakichinja dhabihu katika mahali pa juu, kwa sababu haikuwapo nyumba iliyojengwa kwa jina la BWANA, hata siku zile. Sulemani naye akampenda BWANA, akienda katika amri za Daudi babaye, ila hutoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu. Basi mfalme akaenda Gibeoni, ili atoe dhabihu huko; kwa kuwa ndipo mahali pa juu palipo pakuu. Sulemani akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu ya madhabahu ile. Na huko Gibeoni BWANA akamtokea Sulemani katika ndoto ya usiku; Mungu akamwambia, Omba utakalo nikupe. Sulemani akasema, Umemfanyia mtumwa wako Daudi baba yangu fadhili kuu, kadiri alivyoenenda mbele zako katika kweli, na katika haki, na katika unyofu wa moyo pamoja nawe; nawe umemwekea na fadhili hii kubwa, maana umempa mwana wa kuketi kitini pake kama ilivyo leo. Na sasa, Ee BWANA, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia. Na mtumwa wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa, wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi. Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi? Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili. Mungu akamwambia, Kwa kuwa umeomba neno hili, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako; bali umejitakia akili za kujua kuhukumu; basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe. Na mambo yale usiyoyaomba nimekupa, mali na fahari, hata hapatakuwa na mtu katika wafalme kama wewe, siku zako zote. Nawe ukienda katika njia zangu, na kuyashika mausia yangu, na amri zangu, kama baba yako Daudi alivyokwenda, basi nitazifanya siku zako kuwa nyingi. Naye Sulemani akaamka, na kumbe! Ni ndoto. Akaenda Yerusalemu, akasimama mbele ya sanduku la agano la BWANA, akatoa sadaka za kuteketezwa, akatoa na sadaka za amani; akawafanyia karamu watumishi wake wote.

Soma 1 Fal 3

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 1 Fal 3:1-15