Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Fal 18:15-24

1 Fal 18:15-24 SUV

Eliya akasema, Kama BWANA wa majeshi aishivyo ambaye ninasimama mbele zake, hakika nitajionyesha kwake leo. Basi, Obadia akaenda zake amwone Ahabu, akamwambia; naye Ahabu akaenda kumlaki Eliya. Ikawa, Ahabu alipomwona Eliya, Ahabu akamwambia, Je! Ni wewe, Ewe mtaabishaji wa Israeli? Naye akajibu, Si mimi niliyewataabisha Israeli; bali ni wewe, na nyumba ya baba yako, kwa kuwa mmeziacha amri za BWANA; nawe umewafuata mabaali. Basi sasa upeleke watu, unikusanyie jamii ya Israeli katika mlima wa Karmeli, na wale manabii wa Baali mia nne na hamsini, na wale manabii wa Ashera mia nne, walao chakula mezani pa Yezebeli. Basi, Ahabu akapeleka watu kwa wana wa Israeli wote, akawakusanya manabii pamoja katika mlima wa Karmeli. Naye Eliya akawakaribia watu wote, akanena, Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? BWANA akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno. Ndipo Eliya akawaambia watu, Mimi nimesalia, mimi peke yangu, nabii wa BWANA; lakini manabii wa Baali ni watu mia nne na hamsini. Kwa hiyo na watutolee ng’ombe wawili; wao na wajichagulie ng’ombe mmoja, wamkate-kate na kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeza huyo ng’ombe wa pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini. Nanyi ombeni kwa jina la mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la BWANA; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu. Watu wote wakajibu wakasema, Maneno haya ni mazuri.