Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Fal 18:1-8

1 Fal 18:1-8 SUV

Ikawa baada ya siku nyingi, neno la BWANA likamjia Eliya, katika mwaka wa tatu, kusema, Enenda, ukajionyeshe kwa Ahabu; nami nitaleta mvua juu ya nchi. Basi Eliya akaenda ili ajionyeshe kwa Ahabu. Na njaa ilikuwa nzito katika Samaria. Ahabu akamwita Obadia, aliyekuwa juu ya nyumba yake; (na huyu Obadia alikuwa mwenye kumcha BWANA sana; kwa kuwa ikawa, Yezebeli alipowaua manabii wa BWANA, Obadia akatwaa manabii mia, akawaficha hamsini hamsini katika pango, akawalisha chakula na kuwapa maji). Ahabu akamwambia Obadia, Pita katika nchi, kwenye chemchemi zote za maji, na vijito vyote; labda tutapata majani, tuwahifadhi hai farasi na nyumbu, tusipate hasara ya hao wanyama wote. Basi wakaigawanya nchi, ili wapite katika nchi yote; Ahabu akaenda zake njia moja peke yake, na Obadia akaenda zake njia nyingine peke yake. Na Obadia alipokuwa njiani, kumbe! Eliya akakutana naye. Akamtambua, akaanguka kifudifudi, akanena, Je! Ni wewe, bwana wangu Eliya? Akamjibu, Ni mimi. Enenda, umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo.