Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Fal 18:1-18

1 Fal 18:1-18 SUV

Ikawa baada ya siku nyingi, neno la BWANA likamjia Eliya, katika mwaka wa tatu, kusema, Enenda, ukajionyeshe kwa Ahabu; nami nitaleta mvua juu ya nchi. Basi Eliya akaenda ili ajionyeshe kwa Ahabu. Na njaa ilikuwa nzito katika Samaria. Ahabu akamwita Obadia, aliyekuwa juu ya nyumba yake; (na huyu Obadia alikuwa mwenye kumcha BWANA sana; kwa kuwa ikawa, Yezebeli alipowaua manabii wa BWANA, Obadia akatwaa manabii mia, akawaficha hamsini hamsini katika pango, akawalisha chakula na kuwapa maji). Ahabu akamwambia Obadia, Pita katika nchi, kwenye chemchemi zote za maji, na vijito vyote; labda tutapata majani, tuwahifadhi hai farasi na nyumbu, tusipate hasara ya hao wanyama wote. Basi wakaigawanya nchi, ili wapite katika nchi yote; Ahabu akaenda zake njia moja peke yake, na Obadia akaenda zake njia nyingine peke yake. Na Obadia alipokuwa njiani, kumbe! Eliya akakutana naye. Akamtambua, akaanguka kifudifudi, akanena, Je! Ni wewe, bwana wangu Eliya? Akamjibu, Ni mimi. Enenda, umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo. Akamwambia, Nimekosa nini, hata unitie mimi mtumishi wako mkononi mwa Ahabu, aniue? Kama BWANA, Mungu wako, aishivyo, hakuna taifa wala ufalme ambao bwana wangu hakutuma watu wakutafute; na waliposema, Hayupo, akawaapisha ule ufalme, na taifa, ya kwamba hawakukuona. Nawe sasa wasema, Enenda, umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo. Na itakuwa, mara mimi nikiondoka kwako, roho ya BWANA atakuchukua uende nisikojua; nami nitakapokwenda kumwambia Ahabu, naye asipokuona, ataniua, lakini mimi mtumishi wako namcha BWANA tangu ujana wangu. Je! Bwana wangu hakuambiwa nilivyofanya hapo Yezebeli alipowaua manabii wa BWANA? Jinsi nilivyowaficha manabii wa BWANA, watu mia, hamsini hamsini katika pango, nikawalisha chakula na kuwapa maji? Nawe sasa wasema, Enenda umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo; basi, ataniua. Eliya akasema, Kama BWANA wa majeshi aishivyo ambaye ninasimama mbele zake, hakika nitajionyesha kwake leo. Basi, Obadia akaenda zake amwone Ahabu, akamwambia; naye Ahabu akaenda kumlaki Eliya. Ikawa, Ahabu alipomwona Eliya, Ahabu akamwambia, Je! Ni wewe, Ewe mtaabishaji wa Israeli? Naye akajibu, Si mimi niliyewataabisha Israeli; bali ni wewe, na nyumba ya baba yako, kwa kuwa mmeziacha amri za BWANA; nawe umewafuata mabaali.

Soma 1 Fal 18