1 Yoh 2:18-27
1 Yoh 2:18-27 SUV
Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho. Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu. Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote. Sikuwaandikia ninyi kwa sababu hamwijui iliyo kweli, bali kwa sababu mwaijua, tena kwamba hapana uongo wo wote utokao katika hiyo kweli. Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa Yesu ni Kristo? Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye amkanaye Baba na Mwana. Kila amkanaye Mwana, hanaye Baba; amkiriye Mwana anaye Baba pia. Ninyi basi, hilo mlilolisikia tangu mwanzo na likae ndani yenu. Ikiwa hilo mlilolisikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa ndani ya Mwana, na ndani ya Baba. Na hii ndiyo ahadi aliyotuahidia, yaani, uzima wa milele. Nimewaandikia haya katika habari za watu wale wanaotaka kuwapoteza. Nanyi, mafuta yale mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha; lakini kama mafuta yake yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake.