Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Nya 16:1-36

1 Nya 16:1-36 SUV

Wakaliingiza sanduku la Mungu, na kuliweka katikati ya hema aliyoipiga Daudi kwa ajili yake; wakatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Mungu. Na Daudi alipokwisha kuitoa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani, akawabariki watu kwa jina la BWANA. Kisha akawagawia kila mtu wa Israeli, waume kwa wake, kila mtu mkate wa ngano, na kipande cha nyama, na mkate wa zabibu. Akawaagiza baadhi ya Walawi kwamba watumike mbele ya sanduku la BWANA, wamfanyie ukumbusho, na shukrani, na sifa, BWANA, Mungu wa Israeli; Asafu mkuu wao, na wa pili wake Zekaria, na Yeieli, na Shemiramothi, na Yehieli, na Matithiya, na Eliabu, na Benaya, na Obed-edomu, na Yeieli, wenye vinanda na vinubi; naye Asafu mwenye kupiga matoazi; nao makuhani Benaya na Yahazieli wenye baragumu daima, mbele ya sanduku la agano la Mungu. Ndipo siku hiyo Daudi alipoagiza kwanza kumshukuru BWANA, kwa mkono wa Asafu na nduguze. Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake; Wajulisheni watu matendo yake. Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi; Zitafakarini ajabu zake zote. Jisifuni kwa jina lake takatifu; Na ufurahi moyo wao wamtafutao BWANA. Mtakeni BWANA na nguvu zake; Utafuteni uso wake siku zote. Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya; Miujiza yake na hukumu za kinywa chake; Enyi wazao wa Israeli, mtumishi wake, Enyi wana wa Yakobo, wateule wake. Yeye, BWANA, ndiye Mungu wetu; Duniani mwote mna hukumu zake. Likumbukeni agano lake milele, Neno lile aliloviamuru vizazi elfu. Agano alilofanya na Ibrahimu, Na uapo wake kwa Isaka; Alilomthibitishia Yakobo kuwa amri, Na Israeli liwe agano la milele. Akisema, Nitakupa wewe nchi ya Kanaani, Iwe urithi wenu mliopimiwa; Mlipokuwa watu wawezao kuhesabiwa; Naam, watu wachache na wageni ndani yake. Wakatanga-tanga toka taifa hata taifa, Toka ufalme mmoja hata kwa watu wengine. Hakumwacha mtu awaonee; Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao; Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu. Mwimbieni BWANA, nchi yote; Tangazeni wokovu wake siku kwa siku. Wahubirini mataifa habari za utukufu wake, Na watu wote habari za maajabu yake. Kwa kuwa BWANA ni mkuu mwenye kusifiwa sana; Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote. Maana miungu yote ya watu si kitu; Lakini BWANA ndiye aliyezifanya mbingu. Heshima na adhama ziko mbele zake; Nguvu na furaha zipo mahali pake. Mpeni BWANA, enyi jamaa za watu, Mpeni BWANA utukufu na nguvu. Mpeni BWANA utukufu wa jina lake; Leteni sadaka, mje mbele zake; Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu; Tetemekeni mbele zake, nchi yote. Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike; Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie; Na waseme katika mataifa, BWANA ametamalaki; Bahari na ivume na vyote viijazavyo; Mashamba na yashangilie na vyote vilivyomo; Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha, Mbele za BWANA, Kwa maana anakuja aihukumu nchi. Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Nanyi mkaseme, Ee Mungu wa wokovu wetu, utuokoe, Utukusanye kwa kututoa katika mataifa, Tulishukuru jina lako takatifu, Tuzifanyie shangwe sifa zako. Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, tangu milele hata milele. Na watu wote wakasema, Amina; wakamhimidi BWANA.

Soma 1 Nya 16

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha