Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zekaria 3

3
Maono ya nne: Mavazi safi kwa ajili ya kuhani mkuu
1Kisha akanionesha Yoshua#3:1 Kwa Kiebrania ni Yeshua, maana yake Yehova ni wokovu., kuhani mkuu, akiwa amesimama mbele ya malaika wa Mwenyezi Mungu, naye Shetani amesimama upande wake wa kuume ili amshtaki. 2Mwenyezi Mungu akamwambia Shetani, “Mwenyezi Mungu akukemee Shetani! Mwenyezi Mungu, ambaye ameichagua Yerusalemu, akukemee! Je, mtu huyu siyo kijinga kinachowaka kilichonyakuliwa kwenye moto?”
3Wakati huu, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu alipokuwa amesimama mbele ya malaika. 4Malaika akawaambia wale waliokuwa wamesimama mbele yake, “Mvueni hizo nguo zake chafu.”
Kisha akamwambia Yoshua, “Tazama, nimeiondoa dhambi yako, nami nitakuvika mavazi ya kitajiri.”
5Kisha nikasema, “Mvike kilemba kilicho safi kichwani mwake.” Kwa hiyo wakamvika kilemba safi kichwani na kumvika yale mavazi mengine, wakati malaika wa Mwenyezi Mungu akiwa amesimama karibu.
6Malaika wa Mwenyezi Mungu akamwamuru Yoshua: 7“Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Ikiwa utatembea katika njia zangu na kushika maagizo yangu, basi utaitawala nyumba yangu na kuzilinda nyua zangu, nami nitakupa nafasi miongoni mwa hawa wasimamao hapa.
8“ ‘Sikiliza, ee Yoshua kuhani mkuu, pamoja na wenzako walioketi mbele yako, ambao ni watu walio ishara ya mambo yatakayokuja: Ninaenda kumleta mtumishi wangu, Tawi. 9Tazama, jiwe nililoliweka mbele ya Yoshua! Kuna macho saba juu ya jiwe lile moja, nami nitachora maandishi juu yake,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, ‘nami nitaiondoa dhambi ya nchi hii kwa siku moja.
10“ ‘Katika siku hiyo kila mmoja wenu atamwalika jirani yake akae chini ya mzabibu wake na mtini wake,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.”

Iliyochaguliwa sasa

Zekaria 3: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia