Warumi 12:8-21
Warumi 12:8-21 NEN
kama ni kutia moyo na atie moyo, kama ni kuchangia kwa ajili ya mahitaji ya wengine na atoe kwa ukarimu, kama ni uongozi na aongoze kwa bidii, kama ni kuhurumia wengine na afanye hivyo kwa furaha. Upendo lazima usiwe na unafiki. Chukieni lililo ovu, shikamaneni na lililo jema. Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa ndugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine. Msiwe wavivu, bali mwe na bidii katika roho mkimtumikia Bwana. Kuweni na furaha katika tumaini, katika dhiki kuweni na saburi, dumuni katika maombi. Changieni katika mahitaji ya watakatifu, wakaribisheni wageni. Wabarikini wale wanaowatesa, barikini wala msilaani. Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wale waliao. Kaeni kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, bali mwe tayari kushirikiana na wanyonge. Wala msiwe watu wenye kujivuna kwamba mnajua kila kitu. Msimlipe mtu yeyote ovu kwa ovu. Jitahidini ili mtende yaliyo mema machoni pa watu wote. Kama ikiwezekana, kwa upande wenu kaeni kwa amani na watu wote. Wapendwa, msilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa: “Ni juu yangu kulipiza kisasi, nitalipiza,” asema Bwana. Badala yake: “Kama adui yako ana njaa, mlishe; kama ana kiu, mpe kinywaji. Kwa kufanya hivyo, unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake.” Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.