Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 8

8
Muhuri wa saba na chetezo cha dhahabu
1Mwana-Kondoo alipouvunja ule muhuri wa saba, pakawa kimya mbinguni kwa muda wa nusu saa.
2Nami nikawaona wale malaika saba wanaosimama mbele za Mungu, nao wakapewa tarumbeta saba.
3Malaika mwingine, aliyekuwa na chetezo cha dhahabu, akaja na kusimama mbele ya madhabahu. Akapewa uvumba mwingi ili autoe pamoja na maombi ya watakatifu wote, juu ya yale madhabahu ya dhahabu yaliyo mbele ya kile kiti cha enzi. 4Ule moshi wa uvumba pamoja na yale maombi ya watakatifu, vikapanda juu mbele za Mungu, kutoka mkononi mwa huyo malaika. 5Kisha yule malaika akakichukua kile chetezo, akakijaza moto kutoka kwa yale madhabahu, akautupa juu ya dunia. Pakatokea sauti za radi na ngurumo, miali ya radi na tetemeko la ardhi.
Tarumbeta ya kwanza
6Basi wale malaika saba waliokuwa na zile tarumbeta saba wakajiandaa kuzipiga.
7Malaika wa kwanza akaipiga tarumbeta yake, pakatokea mvua ya mawe na moto uliochanganyika na damu, navyo vikatupwa kwa nguvu juu ya nchi. Na theluthi ya dunia ikateketea, theluthi ya miti ikateketea, na nyasi yote mbichi ikateketea.
Tarumbeta ya pili
8Malaika wa pili akaipiga tarumbeta yake na kitu kama mlima mkubwa unaowaka moto kikatupwa baharini. Theluthi ya bahari ikawa damu, 9theluthi ya viumbe vyenye uhai vilivyoishi baharini vikafa, na theluthi ya meli zikaharibiwa.
Tarumbeta ya tatu
10Malaika wa tatu akaipiga tarumbeta yake, na nyota kubwa iliyokuwa ikiwaka kama taa ikaanguka toka angani, ikaangukia theluthi ya mito na chemchemi za maji. 11Nyota hiyo inaitwa Pakanga#8:11 Pakanga ni mmea chungu sana.. Theluthi ya maji yakawa machungu na watu wengi wakafa kutokana na maji hayo kwa maana yalikuwa machungu.
Tarumbeta ya nne
12Kisha malaika wa nne akaipiga tarumbeta yake, na theluthi ya jua, theluthi ya mwezi na theluthi ya nyota zikapigwa. Kwa hiyo theluthi moja ya mwanga ikawa giza. Theluthi ya mchana ikawa haina mwanga na pia theluthi ya usiku.
13Nilipokuwa tena nikitazama, nikamsikia tai mmoja akipaza sauti kwa nguvu, huku akiruka katikati ya anga, akasema, “Ole! Ole! Ole wa watu wanaoishi duniani, kwa sababu ya tarumbeta ambazo malaika hao wengine watatu wanakaribia kuzipiga!”

Iliyochaguliwa sasa

Ufunuo 8: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia