Ufunuo 6:9-17
Ufunuo 6:9-17 NENO
Mwana-kondoo alipouvunja ule muhuri wa tano, nikaona chini ya madhabahu, roho za wale waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu na kwa ajili ya ushuhuda walioutunza. Wakalia kwa sauti kuu, wakasema, “Hata lini, Ee Bwana Mungu Mwenyezi, uliye mtakatifu na mwaminifu, hutawahukumu na kulipiza kisasi kwa watu wanaoishi duniani kwa ajili ya damu yetu?” Kisha kila mmoja wao akapewa joho jeupe na wakaambiwa wangoje kwa muda kidogo zaidi, hadi idadi ya ndugu zao na watumishi wenzao watakaouawa kama wao walivyouawa, itakapotimia. Nikatazama alipouvunja ule muhuri wa sita. Pakatokea tetemeko kuu la ardhi, na jua likawa jeusi kama gunia lililotengenezwa kwa singa za mbuzi, na mwezi wote ukawa mwekundu kama damu. Nyota zilizo angani zikaanguka ardhini kama vile matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali. Anga ikatoweka kama vile karatasi isokotwavyo, na kila mlima na kila kisiwa kikaondolewa mahali pake. Ndipo wafalme wa dunia, wakuu wote, majemadari, matajiri, wenye nguvu na kila mtu, mtumwa na mtu huru, wakajificha katika mapango na kwenye miamba ya milima. Wakaiita milima na miamba wakisema, “Tuangukieni, mkatufiche na uso wake yeye aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, na mkatuepushe na ghadhabu ya Mwana-Kondoo! Kwa maana siku ile kuu ya ghadhabu yao imewadia. Je, ni nani awezaye kustahimili?”