Ufunuo 6:1-8
Ufunuo 6:1-8 NENO
Nikaangalia Mwana-Kondoo alipofungua ule muhuri wa kwanza miongoni mwa mihuri saba. Ndipo nikasikia mmoja wa wale viumbe wanne wenye uhai akisema kwa sauti kama ya radi: “Njoo!” Nikatazama, na hapo mbele yangu palikuwa na farasi mweupe! Yeye aliyempanda alikuwa na upinde, naye akapewa taji, akampanda akatoka akiwa kama mshindi aelekeaye katika kushinda. Alipouvunja ule muhuri wa pili, nikamsikia yule kiumbe wa pili mwenye uhai akisema, “Njoo!” Ndipo akatokea farasi mwingine mwekundu sana. Yeye aliyempanda akapewa uwezo wa kuondoa amani duniani na kuwafanya watu wauane. Yeye akapewa upanga mkubwa. Mwana-kondoo alipouvunja ule muhuri wa tatu, nikamsikia yule kiumbe wa tatu mwenye uhai akisema, “Njoo!” Nikatazama, na mbele yangu palikuwa na farasi mweusi! Yeye aliyempanda alikuwa na mizani mkononi mwake. Ndipo nikasikia kile kilichokuwa kama sauti katikati ya wale viumbe wanne wenye uhai ikisema, “Kipimo kimoja cha ngano kwa mshahara wa kibarua wa siku moja, na vipimo vitatu vya shayiri kwa mshahara wa kibarua cha siku moja. Lakini usiharibu mafuta wala divai!” Alipouvunja ule muhuri wa nne, nikasikia sauti ya yule kiumbe wa nne mwenye uhai ikisema, “Njoo!” Nikatazama, na hapo mbele yangu palikuwa na farasi mwenye rangi ya kijivujivu! Yeye aliyempanda aliitwa Mauti, naye Kuzimu alikuwa akimfuata nyuma yake kwa karibu. Wakapewa mamlaka juu ya robo ya dunia, kuua kwa upanga, njaa, tauni na kwa wanyama wakali wa dunia.