Ufunuo 6:1-8
Ufunuo 6:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha, nikamwona Mwanakondoo anavunja mhuri mmojawapo wa ile mihuri saba. Nikasikia mmoja wa wale viumbe hai wanne akisema kwa sauti kama ya ngurumo, “Njoo!” Mimi nikatazama, na kumbe palikuwa na farasi mmoja mweupe hapo. Na mpandafarasi wake alikuwa na upinde, akapewa na taji. Basi, akatoka kama mshindi, aendelee kushinda. Kisha, Mwanakondoo akavunja mhuri wa pili. Nikamsikia yule kiumbe hai wa pili akisema, “Njoo!” Nami nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mwingine hapo, mwekundu. Mpandafarasi wake alikabidhiwa jukumu la kuondoa amani duniani, watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa. Kisha Mwanakondoo akavunja mhuri wa tatu. Nikamsikia yule kiumbe hai wa tatu akisema, “Njoo!” Nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mmoja hapo, mweusi. Mpandafarasi wake alikuwa na vipimo viwili vya kupimia uzito mkononi mwake. Nikasikia kitu kama sauti itokayo kwa wale viumbe hai wanne. Nayo ilisema, “Kibaba kimoja cha unga wa ngano kwa kiasi cha fedha denari moja, na vibaba vitatu vya shayiri kwa denari moja. Lakini usiharibu mafuta wala divai!” Kisha, Mwanakondoo akavunja mhuri wa nne. Nikamsikia yule kiumbe hai wa nne akisema, “Njoo!” Nami nikatazama, na kumbe alikuwapo farasi mmoja hapo, rangi yake kijivu. Na jina la mpandafarasi wake lilikuwa Kifo, na Kuzimu alimfuata nyuma. Hao walipewa mamlaka juu ya robo moja ya dunia, wawaue watu kwa upanga, njaa, tauni na kwa wanyama wakali wa dunia.
Ufunuo 6:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha nikaona Mwana-kondoo alipofungua mojawapo ya ile mihuri saba, nikasikia mmoja wa wale wenye uhai wanne akisema, kama kwa sauti ya ngurumo, Njoo! Nikaona, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda ana uta, akapewa taji, naye akatoka, huku akishinda tena apate kushinda. Na alipoufungua mhuri wa pili, nikamsikia yule mwenye uhai wa pili akisema, Njoo! Akatoka farasi mwingine, mwekundu sana, na yeye aliyempanda aliruhusiwa kuiondoa amani katika nchi, ili watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa. Na alipoufungua mhuri wa tatu, nikamsikia yule wa tatu mwenye uhai akisema, Njoo! Nikaona, na tazama, farasi mweusi, na yeye aliyempanda ana mizani mkononi mwake. Nikasikia kama sauti katikati ya hao wenye uhai wanne, ikisema, Kibaba cha ngano kwa nusu rupia, na vibaba vitatu vya shayiri kwa nusu rupia, wala usiyadhuru mafuta wala divai. Na alipoufungua mhuri wa nne, nikasikia sauti ya yule mwenye uhai wa nne akisema, Njoo! Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa wanyama wa nchi.
Ufunuo 6:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha nikaona napo Mwana-Kondoo alipofungua moja ya zile muhuri saba, nikasikia mmoja wa wale wenye uhai wanne akisema, kama kwa sauti ya ngurumo, Njoo! Nikaona, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda ana uta, akapewa taji, naye akatoka, ali akishinda tena apate kushinda. Na alipoifungua muhuri ya pili, nikamsikia yule mwenye uhai wa pili akisema, Njoo! Akatoka farasi mwingine, mwekundu sana, na yeye aliyempanda alipewa kuiondoa amani katika nchi, ili watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa. Na alipoifungua muhuri ya tatu, nikamsikia yule wa tatu mwenye uhai akisema, Njoo! Nikaona, na tazama, farasi mweusi, na yeye aliyempanda ana mizani mkononi mwake. Nikasikia kama sauti katikati ya hao wenye uhai wanne, ikisema, Kibaba cha ngano kwa nusu rupia, na vibaba vitatu vya shayiri kwa nusu rupia, wala usiyadhuru mafuta wala divai. Na alipoifungua muhuri ya nne, nikasikia sauti ya yule mwenye uhai wa nne akisema, Njoo! Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi.
Ufunuo 6:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha nikaangalia wakati Mwana-Kondoo akivunja ile lakiri ya kwanza miongoni mwa zile saba. Ndipo nikasikia mmoja wa wale viumbe wanne wenye uhai akisema kwa sauti kama ya radi: “Njoo!” Nikatazama, na hapo mbele yangu alikuwepo farasi mweupe! Yeye aliyempanda alikuwa na upinde, naye akapewa taji, akampanda akatoka akiwa kama mshindi aelekeaye katika kushinda. Alipoivunja ile lakiri ya pili, nikamsikia yule kiumbe wa pili mwenye uhai akisema, “Njoo!” Ndipo akatokea farasi mwingine mwekundu sana. Yeye aliyempanda akapewa uwezo wa kuondoa amani duniani na kuwafanya watu wauane. Yeye akapewa upanga mkubwa. Mwana-kondoo alipoivunja ile lakiri ya tatu, nikamsikia yule kiumbe wa tatu mwenye uhai akisema, “Njoo!” Nikatazama, na mbele yangu alikuwepo farasi mweusi! Yeye aliyempanda alikuwa na mizani mkononi mwake. Ndipo nikasikia kile kilichokuwa kama sauti katikati ya wale viumbe wanne wenye uhai ikisema, “Kipimo kimoja cha ngano kwa mshahara wa kibarua wa siku moja, na vipimo vitatu vya shayiri kwa mshahara wa kibarua cha siku moja. Lakini usiharibu mafuta wala divai!” Alipovunja ile lakiri ya nne, nikasikia sauti ya yule kiumbe wa nne mwenye uhai ikisema, “Njoo!” Nikatazama, na hapo mbele yangu alikuwepo farasi mwenye rangi ya kijivujivu! Yeye aliyempanda aliitwa Mauti, naye Kuzimu alikuwa akimfuata nyuma yake kwa karibu. Wakapewa mamlaka juu ya robo ya dunia, kuua kwa upanga, njaa, tauni na kwa wanyama wakali wa dunia.