Ufunuo 5:9-14
Ufunuo 5:9-14 NEN
Nao wakaimba wimbo mpya, wakisema: “Wewe unastahili kukitwaa kitabu na kuzivunja lakiri zake, kwa sababu ulichinjwa na kwa damu yako ukamnunulia Mungu watu kutoka kila kabila, kila lugha, kila jamaa na kila taifa. Wewe umewafanya hawa wawe ufalme na makuhani wa kumtumikia Mungu wetu, nao watatawala duniani.” Kisha nikatazama, nikasikia sauti za malaika wengi wakiwa wamekizunguka kile kiti cha enzi, pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne. Idadi yao ilikuwa kumi elfu mara kumi elfu na maelfu ya maelfu. Nao waliimba kwa sauti kuu, wakisema: “Anastahili Mwana-Kondoo, yeye aliyechinjwa, kupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na sifa!” Kisha nikasikia kila kiumbe mbinguni na duniani, chini ya nchi na baharini na vyote vilivyomo ndani yake vikiimba: “Sifa na heshima na utukufu na uweza ni vyake yeye aketiye juu ya hicho kiti cha enzi na kwa Mwana-Kondoo, milele na milele!” Wale viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amen!” Nao wale wazee ishirini na wanne wakaanguka kifudifudi wakaabudu.