Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 66

66
Zaburi 66
Kusifu Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wema wake
Kwa mwimbishaji. Wimbo. Zaburi.
1Mpigieni Mungu kelele za shangwe, dunia yote!
2Imbeni utukufu wa jina lake;
mpeni sifa zake kwa utukufu!
3Mwambieni Mungu, “Jinsi gani
yalivyo ya kutisha matendo yako!
Uwezo wako ni mkuu mno kiasi kwamba
adui wanajikunyata mbele zako.
4Dunia yote yakusujudia,
wanakuimbia wewe sifa,
wanaliimbia sifa jina lako.”
5Njooni mwone yale Mungu aliyoyatenda,
mambo ya kutisha aliyoyatenda
miongoni mwa wanadamu!
6Alifanya bahari kuwa nchi kavu,
wakapita kati ya maji kwa miguu,
njooni, tumshangilie.
7Yeye hutawala kwa uwezo wake milele,
macho yake huangalia mataifa yote:
waasi wasithubutu kujiinua dhidi yake.
8Enyi mataifa, msifuni Mungu wetu,
sauti ya sifa yake isikike,
9ameyahifadhi maisha yetu
na kuizuia miguu yetu kuteleza.
10Ee Mungu, wewe ulitujaribu,
ukatusafisha kama fedha.
11Umetuingiza kwenye nyavu
na umetubebesha mizigo mizito
migongoni mwetu.
12Uliwaruhusu watu watukalie vichwani,
tulipita kwenye moto na kwenye maji,
lakini ulituleta kwenye nchi
iliyojaa utajiri tele.
13Nitakuja hekaluni mwako na sadaka za kuteketezwa
na kukutimizia nadhiri zangu:
14nadhiri ambazo midomo yangu iliahidi
na nilizotamka kwa kinywa changu
nilipokuwa katika shida.
15Nitakutolea dhabihu za wanyama wanono
na sadaka za kondoo dume,
nitakutolea mafahali na mbuzi.
16Njooni msikilize ninyi nyote mnaomcha Mungu,
nami niwaambie aliyonitendea.
17Nilimlilia kwa kinywa changu,
sifa zake zilikuwa katika ulimi wangu.
18Kama ningekuwa nimeyaficha maovu moyoni mwangu,
Bwana asingekuwa amenisikiliza;
19lakini hakika Mungu amenisikiliza
na amesikia sauti yangu katika maombi.
20Ahimidiwe Mungu,
ambaye hakulikataa ombi langu,
wala kunizuilia upendo wake!

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 66: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia