Zaburi 60:1-12
Zaburi 60:1-12 NENO
Ee Mungu, umetukataa na kutokea ghafula juu yetu, umekuwa na hasira; sasa turejeshe! Umetetemesha nchi na kuipasua; uiponye mavunjiko yake, kwa maana inatetemeka. Umewaonesha watu wako nyakati za kukata tamaa; umetunywesha mvinyo unaotuyumbisha. Kwa wale wanaokucha wewe, umewainulia bendera, ili iweze kutwekwa dhidi ya upinde. Tuokoe na utusaidie kwa mkono wako wa kuume, ili wale uwapendao wapate kuokolewa. Mungu amenena kutoka patakatifu pake: “Nitaigawa Shekemu kwa ushindi na kulipima Bonde la Sukothi. Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu; Efraimu ni chapeo yangu, nayo Yuda ni fimbo yangu ya utawala. Moabu ni sinia langu la kunawia, juu ya Edomu natupa kiatu changu; nashangilia kwa kushindwa kwa Ufilisti.” Ni nani atakayenipeleka hadi mji wenye ngome? Ni nani atakayeniongoza hadi nifike Edomu? Ee Mungu, si ni wewe uliyetukataa sisi, na hutoki tena na majeshi yetu? Tuletee msaada dhidi ya adui, kwa maana msaada wa mwanadamu haufai kitu. Kwa msaada wa Mungu tutapata ushindi, naye atawaponda adui zetu.