Zaburi 59
59
Zaburi 59
Kuomba Ulinzi Wa Mungu
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu!” Utenzi wa Daudi. Wakati Sauli alipotuma wapelelezi nyumbani mwa Daudi ili wamuue.
1 Ee Mungu, uniokoe na adui zangu,
unilinde kutokana na hao wanaoinuka dhidi yangu.
2 Uniponye na watu watendao mabaya,
uniokoe kutokana na wamwagao damu.
3 Tazama wanavyonivizia!
Watu wakali wananifanyia hila,
ingawa Ee Bwana, mimi sijakosea
wala kutenda dhambi.
4 Sijatenda kosa; hata hivyo wako tayari kunishambulia.
Inuka unisaidie, uone hali yangu mbaya!
5 Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli!
Zinduka uyaadhibu mataifa yote,
usionyeshe huruma kwa wasaliti.
6 Hurudi wakati wa jioni,
wakibweka kama mbwa,
wakiuzurura mji.
7 Tazama yale wanayotema kutoka vinywa vyao,
hutema upanga kutoka midomo yao,
nao husema, “Ni nani atakayetusikia?”
8 Lakini wewe, Bwana, uwacheke;
unayadharau mataifa hayo yote.
9 Ee nguvu yangu, ninakutazama wewe,
wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu,
10Mungu wangu unipendaye.
Mungu atanitangulia,
naye atanifanya niwachekelee
wale wanaonisingizia.
11 Lakini usiwaue, Ee Bwana, ngao yetu,
au sivyo watu wangu watasahau.
Katika uwezo wako wafanye watangetange
na uwashushe chini.
12 Kwa ajili ya dhambi za vinywa vyao,
kwa ajili ya maneno ya midomo yao,
waache wanaswe katika kiburi chao.
Kwa ajili ya laana na uongo wanaotamka,
13 wateketeze katika ghadhabu,
wateketeze hadi wasiwepo tena.
Ndipo itakapofahamika katika miisho ya dunia
kwamba Mungu anatawala juu ya Yakobo.
14Hurudi jioni,
wakibweka kama mbwa,
wakiuzurura mji.
15 Wanatangatanga wakitafuta chakula,
wasipotosheka hubweka kama mbwa.
16 Lakini mimi nitaziimba nguvu zako,
asubuhi nitaimba juu ya upendo wako;
kwa maana wewe ndiwe ngome yangu
na kimbilio langu wakati wa shida.
17 Ee uliye Nguvu zangu, ninakuimbia sifa.
Wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu,
Mungu unipendaye.
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 59: NEN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.