Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 5:1-12

Zaburi 5:1-12 NENO

Ee Mwenyezi Mungu, tegea sikio maneno yangu, uangalie kupiga kite kwangu. Sikiliza kilio changu ili unisaidie, Mfalme wangu na Mungu wangu, kwa maana kwako ninaomba. Asubuhi, unasikia sauti yangu, Ee Mwenyezi Mungu; asubuhi naleta haja zangu mbele zako, na kusubiri kwa matumaini. Wewe si Mungu unayefurahia uovu, kwako mtu mwovu hataishi. Wenye kiburi hawawezi kusimama mbele yako, unawachukia wote watendao mabaya. Unawaangamiza wasemao uongo. Mwenyezi Mungu huwachukia wanaomwaga damu na wadanganyifu. Lakini mimi, kwa rehema zako kuu, nitakuja katika nyumba yako, kwa unyenyekevu, nitasujudu kulielekea Hekalu lako takatifu. Niongoze katika haki yako, Ee Mwenyezi Mungu, kwa sababu ya adui zangu, nyoosha njia yako mbele yangu. Hakuna neno kinywani mwao linaloweza kuaminika, mioyo yao imejaa maangamizi. Koo lao ni kaburi lililo wazi, kwa ndimi zao, wao hunena udanganyifu. Uwatangaze kuwa wenye hatia, Ee Mungu! Hila zao ziwe anguko lao wenyewe. Wafukuzie mbali kwa sababu ya dhambi zao nyingi, kwa kuwa wamekuasi wewe. Lakini wote wanaokimbilia kwako na wafurahi, waimbe kwa shangwe daima. Ueneze ulinzi wako juu yao, ili wale wanaolipenda jina lako wapate kukushangilia. Kwa hakika, Ee Mwenyezi Mungu, unawabariki wenye haki, unawazunguka kwa wema wako kama ngao.