Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 45

45
Zaburi 45
Wimbo Wa Arusi Ya Kifalme
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa utenzi wa “Yungiyungi.” Utenzi wa wana wa Kora. Wimbo wa arusi.
1Moyo wangu umesisimuliwa na jambo jema
ninapomsimulia mfalme mabeti yangu;
ulimi wangu ni kalamu ya mwandishi stadi.
2 Wewe ni bora kuliko watu wengine wote
na midomo yako imepakwa neema,
kwa kuwa Mungu amekubariki milele.
3 Jifunge upanga wako pajani mwako, ee mwenye nguvu,
jivike fahari na utukufu.
4 Katika fahari yako, songa mbele kwa ushindi,
kwa ajili ya kweli, unyenyekevu na haki,
mkono wako wa kuume na uonyeshe matendo ya kutisha.
5 Mishale yako mikali na ichome mioyo ya adui za mfalme,
mataifa na yaanguke chini ya nyayo zako.
6 Ee Mungu, kiti chako cha enzi
kitadumu milele na milele,
fimbo ya utawala wa haki
itakuwa fimbo ya utawala wa ufalme wako.
7 Unaipenda haki na kuchukia uovu;
kwa hiyo Mungu, Mungu wako,
amekuweka juu ya wenzako,
kwa kukupaka mafuta ya furaha.
8 Mavazi yako yote yana harufu nzuri
ya manemane, udi na mdalasini;
kutoka kwenye majumba ya kifalme
yaliyopambwa kwa pembe za ndovu,
sauti za vinanda vya nyuzi
zinakufanya ufurahi.
9 Binti za wafalme ni miongoni mwa wanawake wako waheshimiwa;
kuume kwako yupo bibi arusi malkia aliyevaa dhahabu ya Ofiri.
10 Sikiliza, ewe binti, fikiri na utege sikio:
Sahau watu wako na nyumba ya baba yako.
11 Mfalme ameshangazwa na uzuri wako;
mheshimu, kwa kuwa yeye ni bwana wako.
12 Binti wa Tiro atakuletea zawadi,
watu wenye utajiri watatafuta upendeleo wako.
13 Utukufu wote una binti mfalme katika chumba chake;
vazi lake limefumwa kwa nyuzi za dhahabu.
14 Anaongozwa kwa mfalme, akiwa amevalia mavazi yaliyotariziwa,
mabikira wenzake wanamfuata
na wanaletwa kwako.
15 Wanaingizwa ndani kwa shangwe na furaha,
na kuingia katika jumba la mfalme.
16 Wana wenu watachukua nafasi za baba zenu,
mtawafanya wakuu katika nchi yote.
17 Nitadumisha kumbukumbu lako katika vizazi vyote,
kwa hiyo mataifa watakusifu milele na milele.

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 45: NEN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha