Zaburi 27:1-6
Zaburi 27:1-6 NEN
BWANA ni nuru yangu na wokovu wangu, nimwogope nani? BWANA ni ngome ya uzima wangu, nimhofu nani? Waovu watakaposogea dhidi yangu ili wanile nyama yangu, adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia, watajikwaa na kuanguka. Hata jeshi linizunguke pande zote, moyo wangu hautaogopa; hata vita vitokee dhidi yangu, hata hapo nitakuwa na ujasiri. Jambo moja ninamwomba BWANA, hili ndilo ninalolitafuta: niweze kukaa nyumbani mwa BWANA siku zote za maisha yangu, niutazame uzuri wa BWANA na kumtafuta hekaluni mwake. Kwa kuwa siku ya shida, atanihifadhi salama katika maskani yake, atanificha uvulini mwa hema yake na kuniweka juu kwenye mwamba. Kisha kichwa changu kitainuliwa juu ya adui zangu wanaonizunguka. Katika maskani yake nitatoa dhabihu kwa kelele za shangwe; nitamwimbia BWANA na kumsifu.