Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 25:1-15

Zaburi 25:1-15 NENO

Kwako wewe, Ee Mwenyezi Mungu, naweka tumaini yangu. Ni wewe ninayekutumainia, Usiniache niaibike, wala adui zangu wanishinde. Kamwe hakuna hata mmoja anayekutegemea atakayeaibishwa, bali wataaibishwa wafanyao hila bila sababu. Nioneshe njia zako, Ee Mwenyezi Mungu, nifundishe mapito yako, niongoze katika kweli yako na kunifundisha, kwa maana wewe ni Mungu Mwokozi wangu, nalo tumaini langu liko kwako wakati wote. Kumbuka, Ee Mwenyezi Mungu, rehema zako kuu na upendo, kwa maana zimekuwepo tangu zamani. Usizikumbuke dhambi za ujana wangu wala njia zangu za uasi, sawasawa na upendo wako unikumbuke, kwa maana wewe ni mwema, Ee Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu ni mwema na mwenye adili, kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia zake. Huwaongoza wanyenyekevu katika haki, naye huwafundisha njia yake. Njia zote za Mwenyezi Mungu ni za upendo na uaminifu kwa wale wanaoshika shuhuda za agano lake. Ee Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya jina lako, unisamehe uovu wangu, ijapokuwa ni mwingi. Ni nani basi, mtu yule anayemcha Mwenyezi Mungu? Atamfundisha katika njia atakayoichagua kwa ajili yake. Mtu huyo atafanikiwa maishani mwake, nao wazao wake watairithi nchi. Siri ya Mwenyezi Mungu iko kwa wale wamchao, yeye huwajulisha agano lake. Macho yangu humwelekea Mwenyezi Mungu daima, kwa kuwa yeye peke yake ndiye ataitoa miguu yangu kutoka mtego.