Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 104:14-27

Zaburi 104:14-27 NEN

Huyafanya majani ya mifugo yaote, na mimea kwa watu kulima, wajipatie chakula kutoka ardhini: divai ya kuufurahisha moyo wa mwanadamu, mafuta kwa ajili ya kungʼarisha uso wake, na mkate wa kutia mwili nguvu. Miti ya BWANA inanyeshewa vizuri, mierezi ya Lebanoni aliyoipanda. Humo ndege hufanya viota vyao, korongo ana nyumba yake kwenye msunobari. Milima mirefu ni makao ya mbuzi-mwitu, majabali ni kimbilio la pelele. Mwezi hugawanya majira, na jua hutambua wakati wake wa kutua. Unaleta giza, kunakuwa usiku, wanyama wote wa mwituni huzurura. Simba hunguruma kwa mawindo yao, na kutafuta chakula chao kutoka kwa Mungu. Jua huchomoza, nao huondoka, hurudi na kulala katika mapango yao. Kisha mwanadamu huenda kazini mwake, katika kazi yake mpaka jioni. Ee BWANA, jinsi matendo yako yalivyo mengi! Kwa hekima ulizifanya zote, dunia imejaa viumbe vyako. Pale kuna bahari, kubwa na yenye nafasi tele, imejaa viumbe visivyo na idadi, vitu vyenye uhai vikubwa na vidogo. Huko meli huenda na kurudi, pia Lewiathani, uliyemuumba acheze ndani yake. Hawa wote wanakutazamia wewe, uwape chakula chao kwa wakati wake.