Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 102

102
Zaburi 102
Maombi ya mtu aliyechoka
Maombi ya mtu aliyechoka. Anapoteseka na kumimina malalamiko yake kwa Mwenyezi Mungu.
1Ee Mwenyezi Mungu, usikie maombi yangu;
kilio changu cha kuomba msaada kikufikie.
2Usinifiche uso wako
ninapokuwa katika shida.
Unitegee sikio lako;
ninapoita, unijibu kwa upesi.
3Kwa kuwa siku zangu zinatoweka kama moshi;
mifupa yangu inaungua kama kaa la moto.
4Moyo wangu umefifia na kunyauka kama jani;
ninasahau kula chakula changu.
5Kwa sababu ya kusononeka kwangu kwa uchungu,
nimebakia ngozi na mifupa.
6Nimekuwa kama bundi wa jangwani,
kama bundi kwenye magofu.
7Nilalapo sipati usingizi;
nimekuwa kama ndege mpweke
kwenye paa la nyumba.
8Mchana kutwa adui zangu hunidhihaki;
wanaonizunguka hutumia jina langu kama laana.
9Ninakula majivu kama chakula changu,
nimechanganya kinywaji changu na machozi
10kwa sababu ya ghadhabu yako kuu,
kwa maana umeniinua na kunitupa kando.
11Siku zangu ni kama kivuli cha jioni,
ninanyauka kama jani.
12Lakini wewe, Ee Mwenyezi Mungu, umeketi kwenye kiti chako cha enzi milele;
sifa zako za ukuu zaendelea vizazi vyote.
13Utainuka na kuihurumia Sayuni,
kwa maana ni wakati wa kumwonesha wema;
wakati uliokubalika umewadia.
14Kwa maana mawe yake ni ya thamani kwa watumishi wako,
vumbi lake lenyewe hulionea huruma.
15Mataifa wataogopa jina la Mwenyezi Mungu,
wafalme wote wa dunia watauheshimu utukufu wako.
16Kwa maana Mwenyezi Mungu ataijenga tena Sayuni
na kutokea katika utukufu wake.
17Ataitikia maombi ya mtu mkiwa,
wala hatadharau hoja yao.
18Hili na liandikwe kwa ajili ya kizazi kijacho,
ili taifa litakaloumbwa baadaye waweze kumsifu Mwenyezi Mungu:
19“Mwenyezi Mungu alitazama chini kutoka patakatifu pake palipo juu,
alitazama dunia kutoka mbinguni,
20kusikiliza vilio vya uchungu vya wafungwa,
na kuwaweka huru wale waliohukumiwa kufa.”
21Kwa hiyo jina la Mwenyezi Mungu latangazwa huko Sayuni
na sifa zake katika Yerusalemu,
22wakati mataifa na falme zitakapokusanyika
ili kumwabudu Mwenyezi Mungu.
23Katika kuishi kwangu alivunja nguvu zangu,
akafupisha siku zangu.
24Ndipo niliposema:
“Ee Mungu wangu, usinichukue katikati ya siku zangu;
miaka yako inaendelea vizazi vyote.
25Hapo mwanzo uliweka misingi ya dunia,
nazo mbingu ni kazi ya mikono yako.
26Hizi zitatoweka, lakini wewe utadumu,
zote zitachakaa kama vazi.
Utazibadilisha kama nguo
nazo zitaondoshwa.
27Lakini wewe, U yeye yule,
nayo miaka yako haikomi kamwe.
28Watoto wa watumishi wako wataishi mbele zako;
wazao wao wataimarishwa mbele zako.”

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 102: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia