Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 8

8
Wito Wa Hekima
1 Je, hekima haitani?
Je, ufahamu hapazi sauti?
2Juu ya miinuko karibu na njia,
penye njia panda, ndipo asimamapo;
3 kando ya malango yaelekeayo mjini,
kwenye maingilio, hulia kwa sauti kubwa, akisema:
4 “Ni ninyi wanaume, ninaowaita;
ninapaza sauti yangu kwa wanadamu wote.
5 Ninyi ambao ni wajinga, pateni akili;
ninyi mlio wapumbavu, pateni ufahamu.
6 Sikilizeni, kwa maana nina mambo muhimu ya kusema;
ninafungua midomo yangu kusema lililo sawa.
7 Kinywa changu husema lililo kweli,
kwa maana midomo yangu huchukia uovu.
8Maneno yote ya kinywa changu ni haki;
hakuna mojawapo lililopotoka wala ukaidi.
9Kwa wenye kupambanua yote ni sahihi;
hayana kasoro kwa wale wenye maarifa.
10 Chagua mafundisho yangu badala ya fedha,
maarifa badala ya dhahabu safi,
11 kwa maana hekima ina thamani kuliko marijani
na hakuna chochote unachohitaji kinacholingana naye.
12 “Mimi hekima, nakaa pamoja na busara;
ninamiliki maarifa na busara.
13 Kumcha Bwana ni kuchukia uovu;
ninachukia kiburi na majivuno,
tabia mbaya na mazungumzo potovu.
14 Ushauri na hukumu sahihi ni vyangu;
nina ufahamu na nina nguvu.
15 Kwa msaada wangu wafalme hutawala
na watawala hutunga sheria zilizo za haki,
16 kwa msaada wangu wakuu hutawala,
na wenye vyeo wote watawalao dunia.
17 Nawapenda wale wanipendao,
na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.
18 Utajiri na heshima viko kwangu,
utajiri udumuo na mafanikio.
19 Tunda langu ni bora kuliko dhahabu safi;
kile nitoacho hupita fedha iliyo bora.
20Natembea katika njia ya unyofu
katika mapito ya haki,
21 nawapa utajiri wale wanipendao
na kuzijaza hazina zao.
22Bwana aliniumba mwanzoni mwa kazi yake,
kabla ya matendo yake ya zamani;
23 niliteuliwa tangu milele,
tangu mwanzoni, kabla ya dunia kuumbwa.
24 Wakati hazijakuwepo bahari, nilikwishazaliwa,
wakati hazijakuwepo chemchemi zilizojaa maji;
25 kabla milima haijawekwa mahali pake,
kabla vilima havijakuwepo, nilikwishazaliwa,
26 kabla hajaumba dunia wala mashamba yake
au vumbi lolote la dunia.
27 Nilikuwepo alipoziweka mbingu mahali pake,
wakati alichora mstari wa upeo wa macho
juu ya uso wa kilindi,
28 wakati aliweka mawingu juu
na kuziweka imara chemchemi za bahari,
29 wakati aliiwekea bahari mpaka wake
ili maji yasivunje agizo lake,
na wakati aliweka misingi ya dunia.
30Wakati huo nilikuwa fundi stadi kando yake.
Nilijazwa na furaha siku baada ya siku,
nikifurahi daima mbele zake,
31 nikifurahi katika dunia yake yote
nami nikiwafurahia wanadamu.
32 “Basi sasa wanangu, nisikilizeni;
heri wale wanaozishika njia zangu.
33Sikilizeni mafundisho yangu mwe na hekima;
msiyapuuze.
34 Heri mtu yule anisikilizaye mimi,
akisubiri siku zote malangoni mwangu,
akingoja kwenye vizingiti vya mlango wangu.
35 Kwa maana yeyote anipataye mimi amepata uzima
na kujipatia kibali kutoka kwa Bwana.
36 Lakini yeyote ashindwaye kunipata
hujiumiza mwenyewe;
na wote wanichukiao mimi hupenda mauti.”

Iliyochaguliwa sasa

Mithali 8: NEN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha