Mithali 6:1-19
Mithali 6:1-19 NEN
Mwanangu, kama umekuwa mdhamini wa jirani yako, ikiwa umeshika mikono kwa kuweka ahadi kwa ajili ya mwingine, kama umetegwa na ulichosema, umenaswa kwa maneno ya kinywa chako, basi fanya hivi mwanangu, ili ujiweke huru, kwa kuwa umeanguka mikononi mwa jirani yako: Nenda ukajinyenyekeshe kwake; msihi jirani yako! Usiruhusu usingizi machoni pako, usiruhusu kope zako zisinzie. Jiweke huru, kama swala mkononi mwa mwindaji, kama ndege kutoka kwenye mtego wa mwindaji. Ewe mvivu, mwendee mchwa; zitafakari njia zake ukapate hekima! Kwa maana yeye hana msimamizi, wala mwangalizi, au mtawala, lakini hujiwekea akiba wakati wa kiangazi na hukusanya chakula chake wakati wa mavuno. Ewe mvivu, utalala hata lini? Utaamka lini kutoka usingizi wako? Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, bado kukunja mikono kidogo upate kupumzika: hivyo umaskini utakuja juu yako kama mnyangʼanyi, na kupungukiwa kutakujia kama mtu mwenye silaha. Mtu mbaya sana na mlaghai, ambaye huzungukazunguka na maneno ya upotovu, ambaye anakonyeza kwa jicho lake, anayetoa ishara kwa miguu yake na kuashiria kwa vidole vyake, ambaye hupanga ubaya kwa udanganyifu moyoni mwake: daima huchochea fitina. Kwa hiyo maafa yatamkumba ghafula; ataangamizwa mara, pasipo msaada. Kuna vitu sita anavyovichukia BWANA, naam, viko saba vilivyo chukizo kwake: macho ya kiburi, ulimi udanganyao, mikono imwagayo damu isiyo na hatia, moyo uwazao mipango miovu, miguu iliyo myepesi kukimbilia uovu, shahidi wa uongo ambaye humwaga uongo, na mtu ambaye huchochea fitina kati ya ndugu.