Mithali 4:7-22
Mithali 4:7-22 NEN
Hekima ni bora kuliko vitu vyote; kwa hiyo jipe hekima. Hata ikikugharimu vyote ulivyo navyo, pata ufahamu. Mstahi, naye atakukweza; mkumbatie, naye atakuheshimu. Atakuvika shada la neema kichwani mwako na kukupa taji ya utukufu.” Sikiliza mwanangu, kubali ninachokuambia, nayo miaka ya maisha yako itakuwa mingi. Ninakuongoza katika njia ya hekima na kukuongoza katika mapito yaliyonyooka. Utembeapo, hatua zako hazitazuiliwa; ukimbiapo, hutajikwaa. Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; mshike, maana yeye ni uzima wako. Usiuweke mguu wako katika njia ya waovu wala usitembee katika njia ya watu wabaya. Epukana nayo, usisafiri katika njia hiyo; achana nayo, na uelekee njia yako. Kwa kuwa hawawezi kulala mpaka watende uovu; wanashindwa hata kusinzia mpaka wamwangushe mtu. Wanakula mkate wa uovu, na kunywa mvinyo wa jeuri. Njia ya wenye haki ni kama nuru ya kwanza ya mapambazuko, ambayo hungʼaa zaidi na zaidi mpaka mchana mkamilifu. Lakini njia ya waovu ni kama giza nene; hawajui kinachowafanya wajikwae. Mwanangu, yasikilize kwa makini yale ninayokuambia; sikiliza kwa makini maneno yangu. Usiruhusu yaondoke machoni pako, yahifadhi ndani ya moyo wako; kwa sababu ni uzima kwa wale wanaoyapata na afya kwa mwili wote wa mwanadamu.