Mithali 3:13-26
Mithali 3:13-26 NENO
Heri mtu yule apataye hekima, mtu yule apataye ufahamu, kwa maana hekima ana faida kuliko fedha na mapato yake ni bora kuliko ya dhahabu safi. Hekima ana thamani kuliko marijani; hakuna chochote unachokitamani kinachoweza kulinganishwa naye. Maisha marefu yako katika mkono wake wa kuume; katika mkono wake wa kushoto kuna utajiri na heshima. Njia zake zinapendeza, mapito yake yote ni amani. Yeye ni mti wa uzima kwa wale wanaomkumbatia; wale wamshikao watabarikiwa. Kwa hekima Mwenyezi Mungu aliiweka misingi ya dunia, kwa ufahamu aliziweka mbingu mahali pake; kwa maarifa yake vilindi viligawanywa, nayo mawingu yanadondosha umande. Mwanangu, hifadhi maamuzi mema na busara, usiache vitoke machoni pako; ndipo vitakapokuwa uzima nafsini mwako na pambo la neema shingoni mwako. Kisha utaenda katika njia yako salama, wala mguu wako hautajikwaa; unapolala, hutaogopa; unapolala, usingizi wako utakuwa mtamu. Usiogope maafa ya ghafula au maangamizi yanayowapata waovu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu atakuwa tumaini lako na kuepusha mguu wako kunaswa katika mtego.