Methali 3:13-26
Methali 3:13-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Heri mtu anayegundua hekima, mtu yule anayepata ufahamu. Hekima ni bora kuliko fedha, ina faida kuliko dhahabu. Hekima ina thamani kuliko johari, hamna unachotamani kiwezacho kulingana nayo. Kwa mkono wake wa kulia Hekima atakupa maisha marefu; kwa mkono wake wa kushoto atakupa mali na heshima. Njia zake ni za kupendeza, zote zaelekea kwenye amani. Hekima ni mti wa uhai kwa wote wampatao; wana heri wote wanaoshikamana naye. Kwa hekima Mwenyezi-Mungu aliweka misingi ya dunia, kwa akili aliziimarisha mbingu. Kwa maarifa yake vilindi vilipasuka, na mawingu yakadondosha umande. Mwanangu, zingatia hekima safi na busara; usiviache vitoweke machoni pako, navyo vitakuwa uhai nafsini mwako, na pambo zuri shingoni mwako. Hapo utaweza kwenda zako kwa usalama, wala mguu wako hautajikwaa. Ukiketi hutakuwa na hofu; ukilala utapata usingizi mtamu. Usiogope juu ya tishio la ghafla, wala shambulio kutoka kwa waovu, Maana Mwenyezi-Mungu ndiye atakayekutegemeza; atakuepusha usije ukanaswa mtegoni.
Methali 3:13-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Heri mtu yule aonaye hekima, Na mtu yule apataye ufahamu. Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha, Na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi. Yeye ana thamani kuliko marijani, Wala vyote uvitamanivyo havilingani naye. Ana wingi wa siku katika mkono wake wa kulia, Utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto. Njia zake ni njia za kupendeza sana, Na mapito yake yote ni amani. Yeye ni mti wa uzima kwao wamshikao sana; Ana heri kila mtu anayeshikamana naye. Kwa hekima BWANA aliiweka misingi ya nchi; Kwa akili zake akazifanya mbingu imara; Kwa maarifa yake vilindi viligawanyika; Na mawingu yadondoza umande. Mwanangu, yasiondoke haya machoni pako, Shika hekima kamili na busara. Basi yatakuwa uzima kwa nafsi yako, Na neema shingoni mwako. Ndipo utakapokwenda katika njia yako salama, Wala mguu wako hautakwaa. Ulalapo hutaona hofu; Naam, utalala na usingizi wako utakuwa mtamu. Usiogope hofu ya ghafla, Wala uharibifu wa waovu utakapofika. Kwa kuwa BWANA atakuwa tumaini lako, Naye atakulinda mguu wako usinaswe.
Methali 3:13-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Heri mtu yule aonaye hekima, Na mtu yule apataye ufahamu. Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha, Na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi. Yeye ana thamani kuliko marijani, Wala vyote uvitamanivyo havilingani naye. Ana wingi wa siku katika mkono wake wa kuume, Utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto. Njia zake ni njia za kupendeza sana, Na mapito yake yote ni amani. Yeye ni mti wa uzima kwao wamshikao sana; Ana heri kila mtu ashikamanaye naye. Kwa hekima BWANA aliiweka misingi ya nchi; Kwa akili zake akazifanya mbingu imara; Kwa maarifa yake vilindi viligawanyika; Na mawingu yadondoza umande. Mwanangu, yasiondoke haya machoni pako, Shika hekima kamili na busara. Basi yatakuwa uzima kwa nafsi yako, Na neema shingoni mwako. Ndipo utakapokwenda katika njia yako salama, Wala mguu wako hautakwaa. Ulalapo hutaona hofu; Naam, utalala na usingizi wako utakuwa mtamu. Usiogope hofu ya ghafula, Wala uharibifu wa waovu utakapofika. Kwa kuwa BWANA atakuwa tumaini lako, Naye atakulinda mguu wako usinaswe.
Methali 3:13-26 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Heri mtu yule apataye hekima, mtu yule apataye ufahamu, kwa maana hekima ana faida kuliko fedha na mapato yake ni bora kuliko ya dhahabu safi. Hekima ana thamani kuliko marijani; hakuna chochote unachokitamani kinachoweza kulinganishwa naye. Maisha marefu yako katika mkono wake wa kuume; katika mkono wake wa kushoto kuna utajiri na heshima. Njia zake zinapendeza, mapito yake yote ni amani. Yeye ni mti wa uzima kwa wale wanaomkumbatia; wale wamshikao watabarikiwa. Kwa hekima BWANA aliiweka misingi ya dunia, kwa ufahamu aliziweka mbingu mahali pake; kwa maarifa yake vilindi viligawanywa, nayo mawingu yanadondosha umande. Mwanangu, hifadhi maamuzi mema na busara, usiache vitoke machoni pako; ndipo vitakapokuwa uzima nafsini mwako na pambo la neema shingoni mwako. Kisha utaenda katika njia yako salama, wala mguu wako hautajikwaa; unapolala, hutaogopa; unapolala, usingizi wako utakuwa mtamu. Usiogope maafa ya ghafula au maangamizi yanayowapata waovu, kwa kuwa BWANA atakuwa tumaini lako na kuepusha mguu wako kunaswa katika mtego.