Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 28

28
1 Mtu mwovu hukimbia ingawa hakuna yeyote anayemfukuza,
bali wenye haki ni wajasiri kama simba.
2Wakati nchi inapokuwa na uasi, inakuwa na viongozi wengi,
bali mwenye ufahamu na maarifa hudumisha utaratibu.
3 Mtu maskini amwoneaye yeye aliye maskini zaidi
ni kama mvua ya dhoruba isiyosaza mazao.
4 Wale waiachao sheria huwasifu waovu,
bali wale waishikao sheria huwapinga.
5 Watu wabaya hawaelewi haki,
bali wale wamtafutao Bwana wanaielewa kikamilifu.
6 Afadhali maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama
kuliko tajiri ambaye njia zake ni potovu.
7 Yeye ashikaye sheria ni mwana mwenye ufahamu,
bali rafiki wa walafi humwaibisha baba yake.
8 Yeye aongezaye utajiri wake kwa riba kubwa mno
hukusanya kwa ajili ya mwingine,
ambaye atawahurumia maskini.
9 Kama mtu yeyote akikataa kusikia sheria,
hata maombi yake ni chukizo.
10 Yeye ambaye humwongoza mwenye haki kwenye mapito mabaya,
ataanguka kwenye mtego wake mwenyewe,
bali wasio na lawama watapokea urithi mwema.
11Mtu tajiri anaweza kuwa na hekima machoni pake mwenyewe,
bali mtu maskini mwenye ufahamu atamfichua.
12 Mwenye haki ashindapo, kuna furaha kubwa,
bali waovu watawalapo, watu hujificha.
13 Yeye afichaye dhambi zake hatafanikiwa,
bali yeyote aziungamaye na kuziacha hupata rehema.
14 Amebarikiwa mtu ambaye siku zote humcha Bwana,
bali yeye afanyaye moyo wake kuwa mgumu
huangukia kwenye taabu.
15Kama simba angurumaye au dubu ashambuliaye,
ndivyo alivyo mtu mwovu atawalaye wanyonge.
16Mtawala dhalimu hana akili,
bali yeye achukiaye mapato ya udhalimu
atafurahia maisha marefu.
17 Mtu mwenye kusumbuliwa na hatia ya kuua
atakuwa mtoro mpaka kufa;
mtu yeyote na asimsaidie.
18 Yeye ambaye mwenendo wake hauna lawama
hulindwa salama,
bali yeye ambaye njia zake ni potovu
ataanguka ghafula.
19 Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele,
bali yule afuataye mambo ya upuzi atakuwa na umaskini wa kumtosha.
20 Mtu mwaminifu atabarikiwa sana,
bali yeye atamaniye kupata utajiri kwa haraka
hataacha kuadhibiwa.
21 Kuonyesha upendeleo si vizuri,
hata hivyo mtu atafanya kosa kwa kipande cha mkate.
22 Mtu mchoyo ana tamaa ya kupata utajiri,
naye hana habari kuwa umaskini unamngojea.
23 Yeye amkemeaye mtu mwishoni hupata kibali zaidi,
kuliko mwenye maneno ya kusifu isivyostahili.
24 Yeye amwibiaye babaye au mamaye
na kusema, “Si kosa,”
yeye ni mwenzi wa yule aharibuye.
25 Mtu mwenye tamaa huchochea fitina,
bali yule amtegemeaye Bwana atafanikiwa.
26 Yeye ajitumainiaye mwenyewe ni mpumbavu,
bali yeye atembeaye katika hekima hulindwa salama.
27 Yeye ampaye maskini
hatapungukiwa na kitu chochote,
bali yeye awafumbiaye maskini macho
hupata laana nyingi.
28 Wakati waovu watawalapo,
watu huenda mafichoni,
bali waovu wanapoangamia,
wenye haki hufanikiwa.

Iliyochaguliwa sasa

Mithali 28: NEN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha