Mithali 25:7-17
Mithali 25:7-17 NENO
ni afadhali yeye akuambie, “Njoo huku juu,” kuliko yeye kukuaibisha mbele ya mkuu. Kile ulichokiona kwa macho yako usiharakishe kukipeleka mahakamani, maana utafanya nini mwishoni kama jirani yako atakuaibisha? Ukifanya shauri na jirani yako, usisaliti siri ya mtu mwingine, ama yeye aisikiaye aweza kukuaibisha, na kamwe sifa yako mbaya haitaondoka. Neno lisemwalo kwa wakati ufaao ni kama matunda ya mtofaa ya dhahabu yaliyowekwa kwenye vijalizo vya fedha. Kama vile kipuli cha dhahabu au pambo la dhahabu safi, ndivyo lilivyo karipio la mtu mwenye hekima kwa sikio lisikilizalo. Kama vile ubaridi wa theluji wakati wa mavuno ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwa wale wamtumao, huburudisha roho za bwana zake. Kama vile mawingu na upepo pasipo mvua ndivyo alivyo mtu ajisifuye kwa zawadi ambazo hatoi. Kwa uvumilivu mtawala aweza kushawishiwa, nao ulimi laini unaweza kuvunja mfupa. Ukipata asali, kula kiasi tu cha kukutosha, ukila zaidi, utatapika. Nenda nyumbani mwa jirani yako mara chache; ukizidisha, atakukinai na atakuchukia.