Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 16:1-17

Mithali 16:1-17 NENO

Mipango ya moyoni ni ya mwanadamu, bali jibu la ulimi hutoka kwa Mwenyezi Mungu. Njia zote za mtu huonekana safi machoni pake mwenyewe, bali makusudi hupimwa na Mwenyezi Mungu. Mkabidhi Mwenyezi Mungu lolote ufanyalo, nayo mipango yako itafanikiwa. Mwenyezi Mungu hufanya kila kitu kwa kusudi lake mwenyewe; hata waovu kwa siku ya maangamizi. Mwenyezi Mungu huwachukia sana wote wenye kiburi cha moyo. Uwe na hakika kwa hili: Hawataepuka kuadhibiwa. Kwa upendo na uaminifu uovu huondolewa; kwa kumcha Mwenyezi Mungu mtu hujiepusha na ubaya. Njia za mtu zinapompendeza Mwenyezi Mungu, huwafanya hata adui zake waishi naye kwa amani. Afadhali kitu kidogo pamoja na haki kuliko mapato mengi pamoja na udhalimu. Moyo wa mtu huifikiri njia yake, bali Mwenyezi Mungu huelekeza hatua zake. Midomo ya mfalme huzungumza kwa hekima ya kiungu, wala kinywa chake hakipotoshi haki. Vipimo na mizani za halali hutoka kwa Mwenyezi Mungu; mawe yote ya kupimia yaliyo katika mfuko ameyafanya yeye. Wafalme huchukia sana kutenda maovu, kwa maana kiti cha ufalme hufanywa imara kupitia haki. Wafalme hufurahia midomo ya uaminifu; humthamini mtu asemaye kweli. Ghadhabu ya mfalme ni mjumbe wa mauti, bali mtu mwenye hekima ataituliza. Uso wa mfalme ung’aapo, inamaanisha uhai; upendeleo wake ni kama wingu la mvua wakati wa vuli. Ni bora kiasi gani kupata hekima kuliko dhahabu, kuchagua ufahamu kuliko fedha! Njia kuu ya wanyofu huepuka ubaya; yeye aichungaye njia yake, huchunga maisha yake.