Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 1:1-19

Mithali 1:1-19 NEN

Mithali za Solomoni mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli: Kwa kupata hekima na nidhamu; kwa kufahamu maneno ya busara; kwa kujipatia nidhamu na busara, kufanya lililo sawa, haki na bila kupendelea; huwapa busara wajinga, maarifa na akili kwa vijana; wenye hekima na wasikilize nao waongeze elimu yao, wenye kupambanua na wapate mwongozo; kwa kufahamu mithali na mifano, misemo na vitendawili vya wenye hekima. Kumcha BWANA ndicho chanzo cha maarifa, lakini wapumbavu hudharau hekima na adabu. Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako, wala usiyaache mafundisho ya mama yako. Hayo yatakuwa taji la maua la neema kichwani pako, na mkufu wa kuipamba shingo yako. Mwanangu, kama wenye dhambi wakikushawishi, usikubaliane nao. Kama wakisema, “Twende tufuatane; tukamvizie mtu na kumwaga damu, njoo tukavizie nafsi isiyo na hatia; tuwameze wakiwa hai kama kaburi, wakiwa wazima kama wale wanaotumbukia shimoni. Tutapata aina zote za vitu vya thamani na kujaza nyumba zetu kwa nyara. Njoo ushirikiane nasi, vitu vyote tutakavyopata tutagawana.” Mwanangu, usiandamane nao. Usiweke mguu wako katika njia zao, kwa kuwa miguu yao hukimbilia kwenye dhambi, ni wepesi kumwaga damu. Tazama ni jinsi gani ilivyo kazi bure kutandaza wavu wakati ndege wote wanakuona! Watu hawa huvizia kumwaga damu yao wenyewe; hujivizia tu wenyewe! Huu ndio mwisho wa wote ambao wanajipatia mali kwa hila; huuondoa uhai wa wale wenye mali.