Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hesabu 9

9
Pasaka huko Sinai
1Mwenyezi Mungu akasema na Musa katika Jangwa la Sinai katika mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili baada ya Waisraeli kutoka Misri. Akasema, 2“Waamuru Waisraeli waadhimishe Pasaka katika wakati ulioamriwa. 3Adhimisheni wakati ulioamriwa, yaani wakati wa kuzama jua siku ya kumi na nne ya mwezi huu, kulingana na desturi zake zote na masharti yake.”
4Hivyo Musa akawaambia Waisraeli waiadhimishe Pasaka, 5nao wakafanya hivyo kwenye Jangwa la Sinai wakati wa kuzama jua siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza. Waisraeli wakafanya kila kitu kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa.
6Lakini baadhi yao hawakuweza kuadhimisha Pasaka siku ile kwa sababu walikuwa najisi kwa ajili ya kugusa maiti. Kwa hiyo wakamwendea Musa na Haruni siku ile ile, 7wakamwambia Musa, “Tumekuwa najisi kwa sababu tumegusa maiti, lakini kwa nini tuzuiliwe kumtolea Mwenyezi Mungu sadaka yake pamoja na Waisraeli wengine katika wakati ulioamriwa?”
8Musa akawajibu, “Ngojeni hadi nitafute kile Mwenyezi Mungu anachoagiza kuwahusu ninyi.”
9Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 10“Waambie Waisraeli: ‘Mmoja wenu au wazao wenu wanapokuwa najisi kwa sababu ya maiti au wakiwa safarini, hata hivyo wanaweza kuadhimisha Pasaka ya Mwenyezi Mungu. 11Wataiadhimisha wakati wa kuzama jua siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili. Watamla mwana-kondoo, pamoja na mkate usiotiwa chachu, na mboga chungu. 12Wasibakize chochote hadi asubuhi wala wasivunje mifupa ya mwana-kondoo. Wanapoiadhimisha Pasaka, hawana budi kufuata masharti yote. 13Lakini mtu aliyetakasika na hayuko safarini asipoiadhimisha Pasaka, mtu huyo hana budi kukatiliwa mbali na watu wake kwa sababu hakutoa sadaka ya Mwenyezi Mungu kwa wakati ulioamriwa. Mtu huyo atawajibika kubeba matokeo ya dhambi yake.
14“ ‘Mgeni anayeishi miongoni mwenu ambaye anataka kuiadhimisha Pasaka ya Mwenyezi Mungu, lazima afanye hivyo kwa kufuata desturi na masharti. Lazima masharti yawe sawasawa kwa mgeni na mzawa.’ ”
Wingu la moto juu ya Maskani
(Kutoka 40:34-38)
15Katika siku hiyo ambayo Maskani, Hema la Ushuhuda, iliposimamishwa, wingu liliifunika. Kuanzia jioni hadi asubuhi wingu lililokuwa juu ya Maskani lilionekana kama moto. 16Hivyo ndivyo lilivyoendelea kuwa; wingu liliifunika wakati wa mchana, na usiku lilionekana kama moto. 17Wakati wowote wingu lilipoinuka kutoka juu ya Hema, nao Waisraeli waliondoka; mahali popote wingu lilipotua, Waisraeli walipiga kambi. 18Kwa amri ya Mwenyezi Mungu Waisraeli waliondoka, na kwa amri yake walipiga kambi. Kwa muda wote wingu lilipokaa juu ya Maskani, Waisraeli walibaki kambini.
19Wingu lilipobaki juu ya Maskani kwa muda mrefu, Waisraeli walitii amri ya Mwenyezi Mungu nao hawakuondoka. 20Wakati mwingine wingu lilikuwa juu ya Maskani kwa siku chache tu; kwa amri ya Mwenyezi Mungu wangepiga kambi na kisha kwa amri yake wangeondoka. 21Wakati mwingine wingu lilikaa kuanzia jioni hadi asubuhi tu; lilipoinuka asubuhi, nao waliondoka. Iwe ni mchana au usiku, wakati wowote wingu lilipoinuka, waliondoka. 22Ikiwa wingu lilikaa juu ya Maskani kwa siku mbili au mwezi au mwaka, Waisraeli wangebaki wamepiga kambi na hawakuondoka; lakini lilipoinuka, wangeondoka.
23Kwa amri ya Mwenyezi Mungu walipiga kambi, na kwa amri ya Mwenyezi Mungu waliondoka. Walitii amri ya Mwenyezi Mungu, kufuatana na agizo lake kupitia Musa.

Iliyochaguliwa sasa

Hesabu 9: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia