Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hesabu 31

31
Kulipiza kisasi juu ya Wamidiani
1Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 2“Uwalipize kisasi Wamidiani kwa ajili ya Waisraeli. Halafu baada ya hayo, utakufa.”
3Kwa hiyo Musa akawaambia watu, “Waandaeni baadhi ya wanaume wenu waende vitani kupigana na Wamidiani ili wawalipize kisasi cha Mwenyezi Mungu. 4Peleka wanaume elfu moja vitani kutoka kila kabila la Israeli.” 5Kwa hiyo waliandaliwa wanaume elfu kumi na mbili kwa vita, wanaume elfu moja kutoka kila kabila, walitolewa kutoka koo za Israeli. 6Musa aliwatuma vitani, watu elfu moja kutoka kila kabila, pamoja na Finehasi mwana wa kuhani Eleazari, ambaye alichukua vyombo vya mahali patakatifu na tarumbeta za kuashiria.
7Walipigana dhidi ya Wamidiani, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa, nao waliua kila mwanaume. 8Miongoni mwa watu waliouawa walikuwa wafalme watano wa Midiani: Evi, Rekemu, Suri, Huri na Reba. Vilevile walimuua Balaamu mwana wa Beori kwa upanga. 9Waisraeli waliwateka wanawake wa Midiani pamoja na watoto wao, na wakachukua makundi ya ng’ombe, kondoo na mali yao kama nyara. 10Walichoma moto miji yote ambayo Wamidiani walikuwa wanaishi, pamoja na kambi zao zote. 11Walichukua nyara zote na mateka, pamoja na watu na wanyama, 12nao waliwaleta wafungwa mateka na nyara kwa Musa na kwa kuhani Eleazari, nao Waisraeli walikusanyika kwenye kambi zao katika tambarare za nchi ya Moabu, kando ya Yordani, ng’ambo ya Yeriko.
13Musa, kuhani Eleazari na viongozi wote wa jumuiya wakatoka kuwalaki nje ya kambi. 14Musa aliwakasirikia maafisa wa jeshi, yaani hao wakuu wa jeshi wa maelfu na wakuu wa jeshi wa mamia, ambao walirudi kutoka vitani.
15Musa akawauliza, “Je, mmewaacha wanawake wote hai? 16Wanawake hao ndio waliofuata ushauri wa Balaamu, nao ndio waliowasababisha Waisraeli wamwasi Mwenyezi Mungu kwa kile kilichotokea kule Peori, na kwa hiyo pigo liliwapata watu wa Mwenyezi Mungu. 17Sasa waue wavulana wote. Pia muue kila mwanamke ambaye alikwisha fanya tendo la ndoa, 18lakini mwacheni hai kwa ajili yenu kila msichana ambaye hajawahi kulala na mwanaume.
19“Ninyi nyote ambao mmeua mtu yeyote au kumgusa mtu ambaye ameuawa, lazima mkae nje ya kambi kwa muda wa siku saba. Katika siku ya tatu na ya saba lazima mjitakase wenyewe pamoja na wafungwa wenu. 20Takaseni kila vazi pamoja na kila kitu kilichotengenezwa kwa ngozi, kwa singa za mbuzi au kwa mti.”
21Kisha kuhani Eleazari aliwaambia askari waliokuwa wameenda vitani, “Haya ndio matakwa ya sheria ambayo Mwenyezi Mungu alimpa Musa: 22Dhahabu, fedha, shaba, chuma, bati, risasi, 23na kitu kingine chochote ambacho kinaweza kuhimili moto lazima mkipitishe kwenye moto, kisha kitakuwa safi. Lakini ni lazima pia kitakaswe kwa maji ya utakaso. Kitu chochote kisichoweza kuhimili moto lazima kipitishwe kwenye yale maji ya utakaso. 24Katika siku ya saba fueni nguo zenu, nanyi mtakuwa safi. Kisha mtaweza kuingia kambini.”
Kugawanya mateka
25Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 26“Wewe na kuhani Eleazari pamoja na viongozi wa jamaa ya jumuiya mtahesabu watu wote na wanyama ambao walitekwa. 27Gawanyeni hizo nyara kati ya askari ambao walishiriki katika vita na kwa jumuiya. 28Kutoka fungu la wale walioenda kupigana vitani, tenga kama ushuru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kitu kimoja kati ya kila mia tano, ikiwa ni wanadamu, ng’ombe, punda, kondoo au mbuzi. 29Chukua ushuru huu kutoka fungu lao, umpe kuhani Eleazari kuwa sehemu ya Mwenyezi Mungu. 30Kutoka fungu la Waisraeli, chukua kitu kimoja kati ya kila hamsini, ikiwa ni wanadamu, ng’ombe, punda, kondoo, mbuzi au wanyama wengine. Hivyo uwape Walawi, ambao wanawajibika kutunza Maskani ya Mwenyezi Mungu.” 31Kwa hiyo Musa na kuhani Eleazari wakafanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
32Nyara zilizobaki kutoka mateka ambayo askari walichukua ni kondoo elfu mia sita na sabini na tano, 33ng’ombe elfu sabini na mbili, 34punda elfu sitini na moja, 35na wanawake elfu thelathini na mbili ambao hawakuwahi kulala na mwanaume.
36Nusu ya fungu la wale waliopigana vitani lilikuwa:
Kondoo elfu mia tatu na thelathini na saba na mia tano, 37ambao ushuru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ulikuwa kondoo mia sita na sabini na watano (675);
38ng’ombe elfu thelathini na sita, ambao ushuru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ulikuwa ng’ombe sabini na wawili;
39punda elfu thelathini na mia tano, ambao ushuru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ulikuwa punda sitini na mmoja;
40Watu elfu kumi na sita, ambao ushuru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ulikuwa watu thelathini na wawili.
41Musa alimpa kuhani Eleazari ushuru kuwa sehemu ya Mwenyezi Mungu, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
42Ile nusu iliyokuwa ya Waisraeli, ambayo Musa aliitenga kutoka kwa ile ya watu waliopigana vitani, 43nusu iliyokuwa ya jumuiya, ilikuwa kondoo elfu mia tatu na thelathini na saba na mia tano, 44ng’ombe elfu thelathini na sita, 45punda elfu thelathini na mia tano, 46na wanadamu elfu kumi na sita. 47Kutoka hiyo nusu iliyokuwa ya Waisraeli, Musa alichagua moja kati ya kila hamsini ya wanadamu na wanyama, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza, naye aliwapa Walawi, ambao waliwajibika kutunza Maskani ya Mwenyezi Mungu.
48Kisha maafisa waliokuwa juu ya vikosi vya jeshi, wakuu wa jeshi wa maelfu na wakuu wa jeshi wa mamia, walimwendea Musa 49na kumwambia, “Watumishi wako wamehesabu askari walio chini ya amri yetu na hakuna hata mmoja aliyekosekana. 50Kwa hiyo tumeleta sadaka kwa Mwenyezi Mungu ya vyombo vya dhahabu kila mmoja wetu alivyopata, yaani vikuku, bangili, pete za muhuri, vipuli na mikufu, ili kufanya upatanisho kwa ajili yetu mbele za Mwenyezi Mungu.”
51Musa na kuhani Eleazari wakapokea kutoka kwao dhahabu, yaani vyombo vyote vilivyonakshiwa. 52Dhahabu yote kutoka kwa wakuu wa jeshi wa maelfu na wakuu wa jeshi wa mamia ambavyo Musa na kuhani Eleazari walimletea Mwenyezi Mungu kama zawadi ilikuwa shekeli elfu kumi na sita, mia saba na hamsini (16,750)#31:52 Shekeli 16,750 ni sawa na kilo 200.. 53Kila askari alikuwa amejichukulia nyara zake binafsi. 54Musa na kuhani Eleazari walipokea dhahabu kutoka kwa wakuu wa jeshi wa maelfu na wakuu wa jeshi wa mamia, wakazileta katika Hema la Kukutania kama ukumbusho kwa Waisraeli mbele za Mwenyezi Mungu.

Iliyochaguliwa sasa

Hesabu 31: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia