Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hesabu 22

22
Balaki amwita Balaamu
1Kisha Waisraeli wakasafiri katika tambarare za Moabu na kupiga kambi kando ya Mto Yordani, ng’ambo ya Yeriko.
2Basi Balaki mwana wa Sipori, aliona mambo yale yote ambayo Israeli aliwatendea Waamori, 3Moabu aliogopa, kwa kuwa walikuwa watu wengi sana. Hakika, Moabu alijawa na hofu kubwa kwa sababu ya Waisraeli.
4Wamoabu wakawaambia wazee wa Midiani, “Umati huu wa watu unaenda kuramba kila kitu kinachotuzunguka, kama maksai anavyoramba majani ya shambani.”
Kwa hiyo Balaki mwana wa Sipori, aliyekuwa mfalme wa Moabu wakati huo, 5akatuma wajumbe kwenda kumwita Balaamu mwana wa Beori, aliyekuwa huko Pethori, karibu na Mto#22:5 yaani Mto Frati, katika nchi yake ya kuzaliwa. Balaki akasema:
“Taifa limekuja kutoka Misri, nao wamefunika uso wa nchi, nao wamekaa karibu nami. 6Sasa uje kuwalaani watu hawa, kwa kuwa wana nguvu sana kuliko mimi. Kisha huenda nikaweza kuwashinda na kuwatoa nje ya nchi. Kwa kuwa ninajua kwamba, wale unaowabariki wanabarikiwa na wale unaowalaani wanalaaniwa.”
7Wazee wa Moabu na wa Midiani wakaondoka, wakiwa wamechukua ada ya uaguzi. Walipoenda kwa Balaamu, wakamweleza kile Balaki alikuwa amesema.
8Balaamu akawaambia, “Mlale hapa usiku huu, nami nitawaletea jibu lile Mwenyezi Mungu atakalonipa.” Kwa hiyo wakuu wa Moabu wakakaa naye.
9Mungu akamjia Balaamu na kumuuliza, “Watu gani hawa walio pamoja nawe?”
10Balaamu akamwambia Mungu, “Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, alinipelekea ujumbe huu: 11‘Taifa ambalo limekuja kutoka Misri limefunika uso wa nchi. Sasa uje unilaanie hao watu. Kisha huenda nitaweza kupigana nao na kuwafukuza.’ ”
12Lakini Mungu akamwambia Balaamu, “Usiende pamoja nao. Hupaswi kulaani watu hao, kwa kuwa wamebarikiwa.”
13Asubuhi iliyofuata Balaamu akaamka, akawaambia wakuu wa Balaki, “Rudini katika nchi yenu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenikataza nisiende pamoja nanyi.”
14Kwa hiyo wakuu wa Moabu wakarudi kwa Balaki na kumwambia, “Balaamu amekataa kuja pamoja nasi.”
15Kisha Balaki akatuma wakuu wengine, wengi zaidi na wanaoheshimiwa kuliko wale wa kwanza. 16Wakafika kwa Balaamu na kumwambia:
“Balaki mwana wa Sipori amesema hivi: Usiruhusu kitu chochote kikuzuie kuja kwangu, 17kwa sababu nitakulipa vizuri sana na kufanya lolote usemalo. Njoo unilaanie watu hawa.”
18Lakini Balaamu akawajibu, “Hata kama Balaki angenipa jumba lake la kifalme likiwa limejazwa fedha na dhahabu, singeweza kufanya kitu chochote kikubwa au kidogo ili kutenda kitu nje ya agizo la Mwenyezi Mungu, Mungu wangu. 19Mlale hapa usiku huu kama wale wengine walivyofanya, nami nitatafuta ni nini kingine Mwenyezi Mungu atakachoniambia.”
20Usiku ule Mungu akamjia Balaamu na kumwambia, “Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita wewe, nenda nao, lakini ufanye tu lile nitakalokuambia.”
Punda wa Balaamu
21Balaamu akaamka asubuhi, akatandika punda wake akaenda pamoja na wakuu wa Moabu. 22Lakini Mungu alikasirika sana alipoenda, naye malaika wa Mwenyezi Mungu akasimama barabarani kumpinga. Balaamu alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye. 23Punda alipomwona malaika wa Mwenyezi Mungu akiwa amesimama barabarani, na upanga ukiwa mkononi mwake, punda akageukia upande kuelekea shambani. Balaamu akampiga ili amrudishe barabarani.
24Ndipo malaika wa Mwenyezi Mungu akasimama katika njia nyembamba iliyo kati ya mashamba mawili ya mizabibu, yakiwa na kuta pande zote mbili. 25Punda alipomwona malaika wa Mwenyezi Mungu, alijisukumiza karibu na ukuta, na kugandamiza mguu wa Balaamu ukutani. Ndipo Balaamu akampiga tena punda.
26Kisha malaika wa Mwenyezi Mungu akaendelea mbele na kusimama mahali pembamba ambapo hapakuwa na nafasi ya kugeuka mkono wa kulia wala wa kushoto. 27Punda alipomwona malaika wa Mwenyezi Mungu, alilala chini Balaamu angali amempanda, naye Balaamu akakasirika na kumpiga kwa fimbo yake. 28Kisha Mwenyezi Mungu akakifungua kinywa cha punda, akamwambia Balaamu, “Nimekutendea nini kinachokufanya unipige mara hizi tatu?”
29Balaamu akamjibu punda, “Umenifanya mjinga! Kama ningekuwa na upanga mkononi mwangu, ningekuua sasa hivi.”
30Punda akamwambia Balaamu, “Je, mimi si punda wako mwenyewe, ambaye umenipanda siku zote, hadi leo? Je, nimekuwa na tabia ya kufanya hivi kwako?”
Akajibu, “Hapana.”
31Kisha Mwenyezi Mungu akafungua macho ya Balaamu, naye akamwona malaika wa Mwenyezi Mungu amesimama barabarani akiwa ameufuta upanga wake. Balaamu akainama, akaanguka kifudifudi.
32Malaika wa Mwenyezi Mungu akamuuliza Balaamu, “Kwa nini umempiga punda wako mara tatu hizi? Nimekuja kukuzuia kwa sababu njia yako imepotoka mbele yangu. 33Punda aliniona na kunikwepa mara hizi tatu. Kama punda hangenikwepa, hakika ningekuwa nimeshakuua sasa, lakini ningemwacha punda hai.”
34Balaamu akamwambia malaika wa Mwenyezi Mungu, “Nimetenda dhambi. Sikutambua kuwa umesimama barabarani kunizuia. Basi kama haikupendezi, nitarudi.”
35Malaika wa Mwenyezi Mungu akamwambia Balaamu, “Uende na watu hao, lakini useme tu lile nikuambialo.” Kwa hiyo Balaamu akaenda na wale wakuu wa Balaki.
36Balaki aliposikia kuwa Balaamu anakuja, akatoka kumlaki katika mji wa Moabu, katika mpaka wa Mto Arnoni, ukingoni mwa nchi yake. 37Balaki akamwambia Balaamu, “Je, sikukupelekea jumbe za haraka? Kwa nini hukuja kwangu? Hivi kweli mimi siwezi kukulipa?”
38Balaamu akajibu, “Vema, sasa nimekuja kwako. Lakini kwani nina uwezo wa kusema tu chochote? Ni lazima niseme tu kile ambacho Mungu ataweka kinywani mwangu.”
39Kisha Balaamu alienda na Balaki hadi Kiriath-Husothi. 40Balaki akatoa dhabihu ya ng’ombe na kondoo; baadhi yake akampa Balaamu na wakuu waliokuwa pamoja naye. 41Asubuhi iliyofuata Balaki akamchukua Balaamu hadi Bamoth-Baali, na kutoka huko Balaamu akawaona baadhi ya watu.

Iliyochaguliwa sasa

Hesabu 22: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia