Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hesabu 20:1-12

Hesabu 20:1-12 NEN

Katika mwezi wa kwanza jumuiya yote ya Kiisraeli ilifika kwenye Jangwa la Sini, nao wakakaa Kadeshi. Miriamu akafa huko na kuzikwa. Mahali hapo hapakuwa na maji kwa ajili ya jumuiya hiyo, nao wakakusanyika ili kumpinga Mose na Aroni. Watu wakagombana na Mose, na kusema, “Laiti tungelikufa wakati ndugu zetu walipoanguka na kufa mbele za BWANA! Kwa nini mmeileta jumuiya ya BWANA kwenye jangwa hili, ili tufe humu, sisi na mifugo yetu? Kwa nini mmetupandisha kutoka Misri mpaka mahali hapa pa kutisha? Hapa hakuna nafaka wala tini, zabibu au makomamanga. Wala hapa hakuna maji ya kunywa!” Mose na Aroni wakaondoka pale kwenye kusanyiko mpaka kwenye mlango wa Hema la Kukutania na kuanguka kifudifudi, nao utukufu wa BWANA ukawatokea. BWANA akamwambia Mose, “Chukua ile fimbo, na wewe na ndugu yako Aroni mkusanye kusanyiko pamoja. Nena na ule mwamba mbele ya macho yao, nao utatoa maji yake. Utatoa maji kutoka huo mwamba kwa ajili ya jumuiya ili wao na mifugo yao waweze kunywa.” Kwa hiyo Mose akaichukua hiyo fimbo kutoka pale ilipokuwa mbele za BWANA kama alivyomwagiza. Mose na Aroni wakakusanya kusanyiko pamoja mbele ya huo mwamba, naye Mose akawaambia, “Sikilizeni, enyi waasi. Je, ni lazima tuwatoleeni maji kutoka mwamba huu?” Ndipo Mose akainua mkono wake na kuupiga mwamba mara mbili kwa fimbo yake. Maji yakabubujika, nayo jumuiya na mifugo yao wakanywa. Lakini BWANA akamwambia Mose na Aroni, “Kwa sababu hamkuniamini mimi kiasi cha kuniheshimu kama mtakatifu machoni pa Waisraeli, hamtaiingiza jumuiya hii katika nchi ninayowapa.”