Hesabu 2
2
Mpangilio wa kambi za makabila
1Mwenyezi Mungu aliwaambia Musa na Haruni: 2“Waisraeli watapiga kambi zao kuzunguka Hema la Kukutania kwa umbali kiasi, kila mwanaume akiwa chini ya beramu yake, pamoja na bendera ya jamaa yake.”
3Kwa upande wa mashariki kuelekea mawio ya jua,
kambi ya makundi ya Yuda watapiga kambi chini ya beramu yao. Kiongozi wa watu wa Yuda ni Nashoni mwana wa Aminadabu. 4Kundi lake lina watu elfu sabini na nne na mia sita.
5Kabila la Isakari watapiga kambi karibu na Yuda. Kiongozi wa watu wa Isakari ni Nethaneli mwana wa Suari. 6Kundi lake lina watu elfu hamsini na nne na mia nne.
7Kabila la Zabuloni litafuata. Kiongozi wa watu wa Zabuloni ni Eliabu mwana wa Heloni. 8Kundi lake lina watu elfu hamsini na saba na mia nne.
9Wanaume wote walio katika kambi ya Yuda, kufuatana na makundi yao, ni elfu mia moja themanini na sita na mia nne. Wao watatangulia kuondoka.
10Kwa upande wa kusini kutakuwa na
kambi ya makundi ya Reubeni chini ya beramu yao. Kiongozi wa watu wa Reubeni ni Elisuri mwana wa Shedeuri. 11Kundi lake lina watu elfu arobaini na sita na mia tano.
12Kabila la Simeoni watapiga kambi karibu na Reubeni. Kiongozi wa watu wa Simeoni ni Shelumieli mwana wa Surishadai. 13Kundi lake lina watu elfu hamsini na tisa na mia tatu.
14Kabila la Gadi litafuata. Kiongozi wa watu wa Gadi ni Eliasafu mwana wa Deueli. 15Kundi lake lina watu elfu arobaini na tano mia sita na hamsini.
16Wanaume wote walio katika kambi ya Reubeni, kufuatana na makundi yao, ni elfu mia moja hamsini na moja na mia nne na hamsini (151,450). Nao watakuwa nafasi ya pili kuondoka.
17Kisha Hema la Kukutania na kambi ya Walawi vitakuwa katikati ya kambi zote. Wao watasafiri kwa utaratibu ule ule kama walivyopiga kambi, kila mmoja mahali pake mwenyewe chini ya beramu yake.
18Upande wa magharibi kutakuwa na
kambi ya makundi ya Efraimu chini ya beramu yao. Kiongozi wa watu wa Efraimu ni Elishama mwana wa Amihudi. 19Kundi lake lina watu elfu arobaini na mia tano.
20Kabila la Manase litafuata baada ya Efraimu. Kiongozi wa watu wa Manase ni Gamalieli mwana wa Pedasuri. 21Kundi lake lina watu elfu thelathini na mbili na mia mbili.
22Kabila la Benyamini litafuata baada ya Manase. Kiongozi wa watu wa Benyamini ni Abidani mwana wa Gideoni. 23Kundi lake lina watu elfu thelathini na tano na mia nne.
24Wanaume wote walio katika kambi ya Efraimu kufuatana na makundi yao ni elfu mia moja na nane na mia moja. Nao watakuwa nafasi ya tatu kuondoka.
25Upande wa kaskazini kutakuwa na
makundi ya kambi ya Dani, chini ya beramu yao. Kiongozi wa watu wa Dani ni Ahiezeri mwana wa Amishadai. 26Kundi lake lina watu elfu sitini na mbili na mia saba.
27Kabila la Asheri watapiga kambi karibu na Dani. Kiongozi wa watu wa Asheri ni Pagieli mwana wa Okrani. 28Kundi lake lina watu elfu arobaini na moja na mia tano.
29Kabila la Naftali litafuata. Kiongozi wa watu wa Naftali ni Ahira mwana wa Enani. 30Kundi lake lina watu elfu hamsini na tatu na mia nne.
31Wanaume wote walio katika kambi ya Dani ni elfu mia moja hamsini na saba na mia sita. Wao watakuwa wa mwisho kuondoka chini ya beramu yao.
32Hawa ndio Waisraeli, wakiwa wamehesabiwa kufuatana na jamaa zao. Wote walio kambini kwa makundi yao ni watu elfu mia sita na tatu mia tano na hamsini (603,550). 33Hata hivyo, Walawi hawakuhesabiwa pamoja na Waisraeli wengine, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
34Kwa hiyo Waisraeli wakafanya kila kitu Mwenyezi Mungu alichomwamuru Musa. Hivyo ndivyo walivyopiga kambi chini ya beramu zao. Pia hivyo ndivyo walivyoondoka, kila mmoja akiwa na ukoo wake na jamaa yake.
Iliyochaguliwa sasa
Hesabu 2: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.