Hesabu 19
19
Maji ya utakaso
1Mwenyezi Mungu akamwambia Musa na Haruni: 2“Hivi ndivyo sheria ambayo Mwenyezi Mungu ameagiza itakavyo: Waambie Waisraeli wakuletee mtamba mwekundu asiye na dosari wala waa, na ambaye hajapata kufungwa nira. 3Mpeni kuhani Eleazari huyo mtamba; naye atatolewa nje ya kambi na kuchinjwa mbele yake huyo kuhani. 4Kisha kuhani Eleazari atachukua sehemu ya damu yake kwenye kidole chake, na kuinyunyiza mara saba kuelekea upande wa mbele ya Hema la Kukutania. 5Wakati angali akitazama, mtamba huyo atateketezwa: ngozi yake, nyama yake, damu na sehemu zake za ndani. 6Kuhani atachukua kuni za mti wa mwerezi, hisopo na sufu nyekundu, na kuvitupa kwenye huyo mtamba anayeungua. 7Baada ya hayo, kuhani lazima afue nguo zake, na aoge mwili wake kwa maji. Kisha anaweza kurudi kambini, lakini atakuwa najisi hadi jioni. 8Mtu amchomaye huyo mtamba lazima naye pia afue nguo zake na kuoga kwa maji, naye pia atakuwa najisi hadi jioni.
9“Mtu ambaye ametakaswa atakusanya majivu ya mtamba huyo na kuyaweka mahali nje ya kambi palipo safi. Yatahifadhiwa na jumuiya ya Waisraeli kwa matumizi katika maji ya utakaso; ni kwa ajili ya kutakasa kutoka dhambini. 10Mtu akusanyaye majivu ya huyo mtamba ni lazima pia afue nguo zake, kadhalika naye pia atakuwa najisi hadi jioni. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa Waisraeli na kwa wageni wanaoishi miongoni mwao.
11“Mtu yeyote agusaye maiti ya mtu yeyote atakuwa najisi kwa siku saba. 12Ni lazima ajitakase mwenyewe kwa maji katika siku ya tatu na siku ya saba, ndipo atakuwa safi. Lakini kama hatajitakasa mwenyewe katika siku ya tatu na ya saba, hatakuwa safi. 13Mtu yeyote agusaye maiti ya mtu yeyote na kushindwa kujitakasa mwenyewe hunajisi Maskani ya Mwenyezi Mungu. Mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na Israeli. Kwa sababu hajanyunyiziwa maji ya utakaso, yeye ni najisi; unajisi wake unabaki juu yake.
14“Hii ndiyo sheria itumikayo wakati mtu amekufa ndani ya hema: Yeyote aingiaye ndani ya hema hilo na yeyote aliye ndani yake watakuwa najisi kwa muda wa siku saba, 15nacho kila chombo kisicho na kifuniko juu yake kitakuwa najisi.
16“Mtu yeyote aliye nje mahali pa wazi agusaye mtu aliyeuawa kwa upanga au mtu aliyekufa kwa kifo cha kawaida, au mtu yeyote agusaye mfupa wa mtu aliyekufa au kaburi, atakuwa najisi kwa siku saba.
17“Kwa mtu aliye najisi, weka majivu ya sadaka ya utakaso wa dhambi ndani ya chombo, umimine maji safi juu yao. 18Kisha mtu aliyetakasika atachukua hisopo, achovye ndani ya maji, na kunyunyizia hema na vifaa vyote pamoja na watu ambao walikuwamo. Pia ni lazima amnyunyizie mtu yeyote ambaye amegusa mfupa wa mtu aliyekufa, au kaburi, au mtu aliyeuawa, au mtu ambaye amekufa kifo cha kawaida. 19Mtu ambaye ni safi ndiye atakayemnyunyizia yeyote ambaye ni najisi siku ya tatu na siku ya saba, na katika siku ya saba atamtakasa mtu huyo. Mtu ambaye ametakaswa lazima afue nguo zake na kuoga kwa maji, na jioni ile atakuwa safi. 20Lakini ikiwa mtu ambaye ni najisi hakujitakasa mwenyewe, ni lazima akatiliwe mbali na jumuiya, kwa sababu ameinajisi Maskani ya Mwenyezi Mungu. Maji ya utakaso hayajanyunyizwa juu yake, naye ni najisi. 21Hili ni agizo la kudumu kwao.
“Mtu anayenyunyiza yale maji ya utakaso lazima pia afue nguo zake, na yeyote anayegusa maji ya utakaso atakuwa najisi hadi jioni. 22Kitu chochote anachogusa mtu aliye najisi kitakuwa najisi, na yeyote akigusaye huwa najisi hadi jioni.”
Iliyochaguliwa sasa
Hesabu 19: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.