Marko 6
6
Isa akataliwa Nasiri
(Mathayo 13:53-58; Luka 4:16-30)
1Isa akaondoka huko na kwenda mji wa kwao, akiandamana na wanafunzi wake. 2Ilipofika siku ya Sabato, akaanza kufundisha katika sinagogi, na wengi waliomsikia wakashangaa.
Nao wakauliza, “Mtu huyu ameyapata wapi mambo haya yote? Tazama ni hekima ya namna gani hii aliyopewa? Tazama matendo ya miujiza ayafanyayo kwa mikono yake! 3Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu? Na ndugu zake si Yakobo, Yose#6:3 yaani Yusufu, Yuda na Simoni? Dada zake wote si tuko nao hapa kwetu?” Nao wakachukizwa sana kwa ajili yake, wakakataa kumwamini.
4Isa akawaambia, “Nabii hakosi heshima isipokuwa katika mji wake mwenyewe, na miongoni mwa jamaa na ndugu zake, na nyumbani mwake.” 5Hakufanya miujiza yoyote huko isipokuwa kuweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya. 6Naye akashangazwa sana kwa kutoamini kwao.
Isa awatuma wale kumi na wawili
(Mathayo 10:5-15; Luka 9:1-6)
Kisha Isa akawa anaenda kutoka kijiji kimoja hadi kingine akifundisha. 7Akawaita wale kumi na wawili, akawatuma wawili wawili, na kuwapa mamlaka kutoa pepo wachafu.
8Akawaagiza akisema, “Msichukue chochote kwa ajili ya safari isipokuwa fimbo tu. Msichukue mkate, wala mkoba, wala fedha kwenye mikanda yenu. 9Vaeni viatu, lakini msivae nguo ya ziada. 10Mkiingia kwenye nyumba yoyote, kaeni humo hadi mtakapoondoka katika mji huo. 11Kama mahali popote hawatawakaribisha wala kuwasikiliza, mtakapoondoka huko, kung’uteni mavumbi kutoka miguu yenu ili kuwe ushuhuda dhidi yao.”
12Kwa hiyo wakaenenda na kuhubiri kwamba inawapasa watu kutubu na kuacha dhambi. 13Wakatoa pepo wachafu wengi, wakawapaka wagonjwa wengi mafuta na kuwaponya.
Yahya akatwa kichwa
(Mathayo 14:1-12; Luka 9:7-9)
14Mfalme Herode akasikia habari hizi, kwa maana jina la Isa lilikuwa limejulikana sana. Watu wengine walikuwa wakisema, “Yahya amefufuliwa kutoka kwa wafu, ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.”
15Wengine wakasema, “Yeye ni Ilya.”
Nao wengine wakasema, “Yeye ni nabii, kama mmoja wa manabii wa zamani.”
16Lakini Herode aliposikia habari hizi, akasema, “Huyo ni Yahya, niliyemkata kichwa, amefufuliwa kutoka kwa wafu!”
17Herode mwenyewe alikuwa ameagiza kwamba Yahya akamatwe, afungwe na kutiwa gerezani. Alifanya hivi kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake, ambaye Herode alikuwa amemwoa. 18Yahya alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kuwa na mke wa ndugu yako.” 19Kwa hiyo Herodia alikuwa amemwekea Yahya kinyongo, akataka kumuua. Lakini hakuweza, 20kwa sababu Herode alimwogopa Yahya akijua kwamba ni mtu mwenye haki na mtakatifu, hivyo akamlinda. Herode alifadhaika sana alipomsikia Yohana, lakini bado alipenda kumsikiliza.
21Hatimaye Herodia alipata wakati mwafaka aliokuwa akiutafuta. Mfalme Herode alifanya karamu kubwa wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwake. Akawaalika maafisa wake wakuu, majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa Galilaya. 22Binti Herodia alipoingia na kucheza, akamfurahisha Herode pamoja na wageni wake walioalikwa chakulani.
Mfalme Herode akamwambia yule binti, “Niombe kitu chochote utakacho, nami nitakupa.” 23Tena akamwahidi kwa kiapo, akamwambia, “Chochote utakachoomba nitakupa, hata kama ni nusu ya ufalme wangu.”
24Yule binti akatoka nje, akaenda kumuuliza mama yake, “Niombe nini?”
Mama yake akamjibu, “Omba kichwa cha Yahya.”
25Yule binti akarudi haraka kwa mfalme, akamwambia, “Nataka unipe sasa hivi kichwa cha Yahya kwenye sinia.”
26Mfalme akasikitika sana, lakini kwa sababu alikuwa ameapa viapo mbele ya wageni wake, hakutaka kumkatalia. 27Mara mfalme akatuma askari mmoja wa walinzi wake kukileta kichwa cha Yahya. Akaenda na kumkata Yahya kichwa humo gerezani, 28akakileta kichwa chake kwenye sinia na kumpa yule msichana, naye yule msichana akampa mama yake. 29Wanafunzi wa Yahya walipopata habari hizi, wakaja na kuuchukua mwili wake, wakauzika kaburini.
Isa alisha wanaume 5,000
(Mathayo 14:13-21; Luka 9:10-17; Yohana 6:1-14)
30Wale mitume wakakusanyika kwa Isa na kumpa taarifa ya mambo yote waliyokuwa wamefanya na kufundisha. 31Basi kwa kuwa watu wengi mno walikuwa wakija na kutoka, hata wakawa hawana nafasi ya kula, Isa akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni peke yetu mahali pa faragha, mpate kupumzika.”
32Hivyo wakaondoka kwa mashua peke yao, wakaenda mahali pasipo na watu. 33Lakini watu wengi waliowaona wakiondoka, wakawatambua, nao wakaenda haraka kwa miguu kutoka miji yote, nao wakatangulia kufika. 34Isa alipofika kando ya bahari, aliona kundi kubwa la watu, akawahurumia kwa maana walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi.
35Mchana ulipokuwa umeendelea sana, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, nazo saa zimeenda sana. 36Waage watu ili waende mashambani na vijijini jirani, wakajinunulie chakula.”
37Lakini Isa akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.”
Wakamwambia, “Je, twende tukanunue mikate ya dinari mia mbili#6:37 Dinari moja ilikuwa kama mshahara wa kibarua wa siku moja. ili tuwape watu hawa wale?”
38Akawauliza, “Kuna mikate mingapi? Nendeni mkaangalie.”
Walipokwisha kujua, wakarudi, wakamwambia, “Kuna mikate mitano na samaki wawili.”
39Kisha Isa akawaamuru wawaketishe watu makundi makundi kwenye majani, 40nao wakaketi kwenye vikundi vya watu mia mia, na wengine hamsini hamsini. 41Isa akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi wake ili wawagawie wale watu wote. Pia akawagawia wote wale samaki wawili. 42Watu wote wakala, wakashiba. 43Nao wanafunzi wake wakakusanya vipande vilivyosalia vya mikate na samaki, wakajaza vikapu kumi na viwili. 44Idadi ya wanaume waliokula walikuwa elfu tano.
Isa atembea juu ya maji
(Mathayo 14:22-33; Yohana 6:16-21)
45Mara Isa akawaambia wanafunzi wake waingie kwenye mashua wamtangulie kwenda Bethsaida, wakati yeye alikuwa akiwaaga wale watu. 46Baada ya kuwaaga, akaenda mlimani kuomba.
47Ilipofika jioni, ile mashua ilikuwa imefika katikati ya bahari, na Isa alikuwa peke yake katika nchi kavu. 48Akawaona wanafunzi wake wanahangaika na kupiga makasia kwa nguvu, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Isa akawaendea wanafunzi wake, akiwa anatembea juu ya maji. Alikuwa karibu kuwapita, 49lakini walipomwona akitembea juu ya maji, wakadhani ni mzimu. Wakapiga yowe, 50kwa sababu wote walipomwona waliogopa.
Mara Isa akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope!” 51Akapanda ndani ya mashua nao, na ule upepo ukakoma! Wakashangaa kabisa, 52kwa kuwa walikuwa hawajaelewa kuhusu ile mikate. Mioyo yao ilikuwa migumu.
Isa awaponya wagonjwa Genesareti
(Mathayo 14:34-36)
53Walipokwisha kuvuka, wakafika nchi ya Genesareti, wakatia nanga. 54Mara waliposhuka kutoka mashua yao, watu wakamtambua Isa. 55Wakaenda katika vijiji vyote upesi, wakawabeba wagonjwa kwenye mikeka ili kuwapeleka mahali popote waliposikia kuwa Isa yupo. 56Kila mahali Isa alipoenda, iwe vijijini, mijini au mashambani, watu waliwaweka wagonjwa wao masokoni. Wakamwomba awaruhusu hao wagonjwa waguse japo upindo wa vazi lake. Nao wote waliomgusa waliponywa.
Iliyochaguliwa sasa
Marko 6: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.