Marko 6:30-56
Marko 6:30-56 NEN
Wale mitume wakakusanyika kwa Yesu na kumpa taarifa ya mambo yote waliyokuwa wamefanya na kufundisha. Basi kwa kuwa watu wengi mno walikuwa wakija na kutoka, hata wakawa hawana nafasi ya kula, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni peke yetu mahali pa faragha, mpate kupumzika.” Hivyo wakaondoka kwa mashua peke yao, wakaenda mahali pasipo na watu. Lakini watu wengi waliowaona wakiondoka, wakawatambua, nao wakaenda haraka kwa miguu kutoka miji yote, nao wakatangulia kufika. Yesu alipofika kando ya bahari, aliona makutano makubwa ya watu, akawahurumia kwa maana walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi. Mchana ulipokuwa umeendelea sana, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, nazo saa zimekwenda sana. Waage watu ili waende mashambani na vijijini jirani, wakajinunulie chakula.” Lakini Yesu akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.” Wakamwambia, “Je, twende tukanunue mikate ya dinari 200 ili tuwape watu hawa wale?” Akawauliza, “Kuna mikate mingapi? Nendeni mkaangalie.” Walipokwisha kujua wakarudi, wakamwambia, “Kuna mikate mitano na samaki wawili.” Kisha Yesu akawaamuru wawaketishe watu makundi makundi kwenye majani, nao wakaketi kwenye makundi ya watu mia mia na wengine hamsini hamsini. Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi wake ili wawagawie wale watu wote. Pia akawagawia wote wale samaki wawili. Watu wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wake wakakusanya vipande vilivyosalia vya mikate na samaki, wakajaza vikapu kumi na viwili. Idadi ya wanaume waliokula walikuwa 5,000. Mara Yesu akawaambia wanafunzi wake waingie kwenye mashua watangulie kwenda Bethsaida, wakati yeye alikuwa akiwaaga wale makutano. Baada ya kuwaaga wale watu, akaenda mlimani kuomba. Ilipofika jioni, ile mashua ilikuwa imefika katikati ya bahari, na Yesu alikuwa peke yake katika nchi kavu. Akawaona wanafunzi wake wanahangaika na kupiga makasia kwa nguvu, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Yesu akawaendea wanafunzi wake, akiwa anatembea juu ya maji. Alikuwa karibu kuwapita, lakini walipomwona akitembea juu ya maji, wakadhani ni mzimu. Wakapiga yowe, kwa sababu wote walipomwona waliogopa. Mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope!” Akapanda ndani ya mashua nao, na ule upepo ukakoma! Wakashangaa kabisa, kwa kuwa walikuwa hawajaelewa kuhusu ile mikate. Mioyo yao ilikuwa migumu. Walipokwisha kuvuka, wakafika nchi ya Genesareti, wakatia nanga. Mara waliposhuka kutoka mashua yao, watu wakamtambua Yesu. Wakaenda katika vijiji vyote upesi, wakawabeba wagonjwa kwenye mikeka ili kuwapeleka mahali popote waliposikia kuwa Yesu yupo. Kila mahali Yesu alipokwenda, iwe vijijini, mijini au mashambani, watu waliwaweka wagonjwa wao masokoni. Wakamwomba awaruhusu hao wagonjwa waguse japo upindo wa vazi lake. Nao wote waliomgusa waliponywa.