Marko 2:13-17
Marko 2:13-17 NENO
Isa akaenda tena kandokando ya Bahari ya Galilaya. Umati mkubwa wa watu wakamfuata, naye akaanza kuwafundisha. Alipokuwa akitembea, akamwona Lawi mwana wa Alfayo ameketi forodhani mahali pa kutoza ushuru. Isa akamwambia, “Nifuate.” Naye Lawi akaondoka, akamfuata Isa. Isa alipokuwa ameketi akila chakula nyumbani mwa Lawi, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuwa wakila pamoja naye na wanafunzi wake, kwa maana ni watu wengi waliokuwa wakimfuata. Walimu wa Torati waliokuwa Mafarisayo walipomwona akila pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi, wakawauliza wanafunzi wake: “Mbona Isa anakula na watoza ushuru na wenye dhambi?” Isa aliposikia haya akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”