Marko 14:1-11
Marko 14:1-11 NENO
Zilikuwa zimebaki siku mbili tu kabla ya Sikukuu ya Pasaka, na Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Viongozi wa makuhani na walimu wa Torati walikuwa wakitafuta njia ya kumkamata Isa kwa hila na kumuua. Lakini walisema, “Tusilifanye jambo hili wakati wa Sikukuu, maana watu wanaweza wakafanya ghasia.” Isa alikuwa Bethania nyumbani mwa Simoni aliyekuwa na ukoma. Alipokuwa ameketi mezani akila chakula cha jioni, mwanamke mmoja aliingia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa. Akaivunja hiyo chupa, akamiminia hayo manukato kichwani mwa Isa. Baadhi ya watu waliokuwa pale walikasirika na wakasemezana, “Upotevu huu wote wa manukato ni wa nini? Manukato haya yangeuzwa kwa zaidi ya dinari mia tatu, na fedha hizo wakapewa maskini.” Wakamkemea vikali huyo mwanamke. Lakini Isa akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Mwacheni! Yeye amenitendea jambo zuri sana. Maskini mtakuwa nao siku zote na mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaotaka. Lakini mimi hamtakuwa nami siku zote. Huyu mwanamke amenitendea lile aliloweza. Ameumiminia mwili wangu manukato ili kuniandaa kwa maziko yangu. Amin, nawaambia, mahali popote ulimwenguni ambapo Injili itahubiriwa, jambo hili alilolitenda huyu mwanamke litatajwa pia kwa ukumbusho wake.” Kisha Yuda Iskariote, mmoja wa wale wanafunzi kumi na wawili, akaenda kwa viongozi wa makuhani ili kumsaliti Isa kwao. Walifurahi sana kusikia jambo hili na wakaahidi kumpa fedha. Hivyo yeye akawa anatafuta wakati uliofaa wa kumsaliti.