Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 13:14-37

Marko 13:14-37 NENO

“Mtakapoona ‘chukizo la uharibifu’ limesimama mahali pasipolipasa (asomaye na afahamu), basi wale walio Yudea wakimbilie milimani. Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke au kuingia ndani ili kuchukua chochote. Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake. Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo! Ombeni mambo haya yasitokee wakati wa baridi. Kwa maana siku hizo zitakuwa za dhiki kuu ambayo haijapata kuwa tangu mwanzo, hapo Mungu alipoumba ulimwengu, hadi leo, na wala haitakuwa tena kamwe. “Kama Mwenyezi Mungu hangefupisha siku hizo, kamwe hakuna mtu yeyote angeokoka. Lakini kwa ajili ya wateule, wale aliowachagua, amezifupisha siku hizo. Wakati huo mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Al-Masihi huyu hapa!’ au, ‘Tazama, yuko kule,’ msisadiki. Kwa maana watatokea masihi wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara na maajabu ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule. Hivyo jihadharini. Nimekwisha kuwaambia mambo haya yote mapema kabla hayajatukia. “Lakini katika siku hizo, baada ya hiyo dhiki, “ ‘jua litatiwa giza nao mwezi hautatoa nuru yake; nazo nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za anga zitatikisika.’ “Ndipo watu wote watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu. Naye atawatuma malaika wake wawakusanye wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka miisho ya dunia hadi miisho ya mbingu. “Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Matawi yake yanapoanza kuchipua na kutoa majani, mnatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. Vivyo hivyo, myaonapo mambo haya yakitukia, mnatambua kwamba wakati u karibu, hata malangoni. Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. “Kwa habari ya siku ile na saa hakuna yeyote ajuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake. Jihadharini! Kesheni! Kwa maana hamjui wakati ule utakapowadia. Ni kama mtu anayesafiri. Anaiacha nyumba yake na kuwaachia watumishi wake kuiangalia, kila mtu na kazi yake, kisha akamwamuru yule bawabu aliye mlangoni akeshe. “Basi kesheni, kwa sababu hamjui ni lini mwenye nyumba atakaporudi: iwapo ni jioni, au ni usiku wa manane, au alfajiri awikapo jogoo, au mapambazuko, akija ghafula asije akawakuta mmelala. Lile ninalowaambia ninyi, nawaambia watu wote: ‘Kesheni!’ ”