Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 11:20-33

Marko 11:20-33 NENO

Kesho yake asubuhi walipokuwa wakipita, wakauona ule mtini umenyauka kutoka juu hadi kwenye mizizi yake. Petro akakumbuka na kumwambia Isa, “Mwalimu, tazama! Ule mtini ulioulaani umenyauka!” Isa akawajibu, “Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia, mtu yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ng’oka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, atatimiziwa. Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote mtakayoyaomba mkisali, aminini kwamba mmeyapokea, nayo yatakuwa yenu. Nanyi kila msimamapo kusali, sameheni mkiwa na neno na mtu, ili naye Baba yenu aliye mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu. [ Lakini kama ninyi msiposamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]” Wakafika tena Yerusalemu, na Isa alipokuwa akitembea Hekaluni, viongozi wa makuhani, walimu wa Torati pamoja na wazee wa watu wakamjia. Wakamuuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Na ni nani aliyekupa mamlaka ya kufanya hayo?” Isa akawajibu, “Nitawauliza swali moja. Nijibuni, nami nitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya. Je, ubatizo wa Yahya ulitoka mbinguni au kwa wanadamu? Niambieni!” Wakahojiana wao kwa wao na kusema, “Tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona hamkumwamini?’ Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu’ ” (waliwaogopa watu, kwa sababu kila mtu aliamini kwamba Yahya alikuwa nabii wa kweli); kwa hiyo wakamjibu Isa, “Hatujui.” Naye Isa akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.”